Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akizungumza kwenye kilele cha siku ya wanawake Duniani ambazo kimkoa zimefanyika viwanja vya Bandari mjini Mbambabay wilayani Nyasa
Baadhi ya wanawake wa Mkoa wa Ruvuma wakiwa katika maandamano ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambazokimkoa zimefanyika mjini Mbambabay wilayani Nyasa
Na Albano Midelo,Ruvuma
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amekemea mila potofu kwa baadhi ya jamii zinazoendelea kuwakandamiza wanawake na kuwapoka mizania ya haki na usawa.
Kanali Thomas amesema hayo wakati anazungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani ambayo kimkoa yamefanyika katika viwanja vya Bandari mjini Mbambabay wilayani Nyasa.
Amesema vitendo hivyo vinaendelea kusababisha kuwepo kwa lindi la umasikini katika ngazi ya kaya kwa miongo mingi hali inayoathiri malezi na makuzi ya Watoto katika jamii.
Ameongeza kuwa wanawake wengi wananyimwa haki hasa katika umiliki wa rasilimali ardhi,kukosa dhamana za kuwezesha umiliki wa rasilimali ardhi,kukosa dhamana ya upatikanaji wa huduma za kifedha,haki ya kupata elimu na haki ya kuchaguliwa kuwa kiongozi katika ngazi ya jamii.
“Serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imesimama kidete katika kulinda haki na kujenga usawa kwa jamii yote,serikali inahakikisha wanawake wanapata haki na kuwa majasiri katika kujiamini na kujitokeza kugombea na kushinda nafasi mbalimbali za uongozi’’,alisisitiza Kanali Thomas.
Ametoa rai kwa wanawake kutoa taarifa kwa wakati inapotokea unyanyasaji au ukatili wa aina yoyote sanjari na kutoa ushirikiano katika kutoa elimu ya kupinga ukatili na unyanyasaji.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa ameipongeza serikali ya Awamu ya Sita kwa kutoa mikopo isiyokuwa na riba kwa wanawake inayotokana na asilimia kumi ya mapato,ambapo amesema katika Mkoa wa Ruvuma zaidi ya shilingi milioni 588 zimetolewa kwa wanawake katika kipindi cha mwaka 2022/2023.
Awali Risala ya wanawake wa Mkoa wa Ruvuma iliyosomwa na Mariam Juma kwenye maadhimisho hayo imezitaja changamoto zinazoendelea kuwakabili wanawake zikiwemo za kuwepo mfumo dume unaolindwa na mila na desturi potofu katika jamii.
Risala hiyo imezitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni wanawake kukosa haki ya kumiliki ardhi,kupigwa,kubakwa,kutelekezwa na kunyang’anywa mali na ndugu wa mume pindi wanapofiwa na waume zao na kunyimwa haki zao za msingi.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Komred Oddo Mwisho ameipongeza serikali kwa kutekeleza Ilani ya CCM yam waka 2025 ambayo amesema imetelezwa kwa kiwango kikubwa baada ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuleta fedha nyingi za kutekeleza miradi mbalimbali katika Mkoa wa Ruvuma.
Komredi Mwisho pia amempongeza Rais Dkt Samia kwa kuimarisha demokrasia siku ya wanawake duniani ambapo ameungana na wanawake cha CHADEMA kama mgeni rasmi.
Kaulimbiu ya siku ya wanawake Duniani ya mwaka huu inasema Ubunifu na mabadiliko ya teknolojia;chachu katika kuleta usawa wa kijinsia.