Mwenyekiti wa Mtandao wa Askari Polisi wanawake Mkoa wa Mbeya ambaye pia ni Afisa Mnadhimu namba moja Mkoa wa Mbeya ACP CHRISTINA MUSYANI Machi 06, 2023 amewaongoza Askari Polisi wanawake Mkoa wa Mbeya kuwatembelea na kutoa zawadi kwa wanafunzi wa Shule za Sekondari na Msingi zilizopo katika mamlaka ya Mji Mdogo – Makongolosi Wilayani Chunya.
Akizungumza wakati wa utoaji wa taulo za kike, sabuni na vifaa vingine kwa wanafunzi wa Shule za Msingi KIPOKA, NYERERE na MAKONGOLOSI na Shule ya Sekondari KIPOKA, ACP MUSYANI amewataka wanafunzi hao kuhakikisha wanajitunza kwa kutoruhusu miili yao kushikwashikwa mtu yeyote yule ili kujiepusha na vitendo vya ukatili wa kijinsia ambavyo vinaweza kutowesha ndoto zao za kimaisha.
Aidha ACP MUSYANI amewataka wanafunzi hao kutokaa kimya pindi waonapo vitendo vya ukatili wa kijinsia au uhalifu wa aina yoyote, amewataka kutoa taarifa kwa wazazi, walezi au walimu wao kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
Sambamba na hilo, ACP MUSYANI kwa niaba ya mtandao wa Askari Polisi wanawake Mkoa wa Mbeya ameushukuru uongozi wa mamlaka ya Mji Mdogo wa Makongolosi kwa jitihada za makusudi za kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Naye Mhe. Diwani wa Kata ya Bwawani SAIRON MBALAWATA PASHILA amelishukuru kipekee Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kuwakumbuka wanafunzi wa Shule za Sekondari na Msingi zilizopo katika mamlaka ya Mji Mdogo wa Makongolosi. Pia amewahakikisha kuwa zawadi walizotoa zitakwenda kupunguza changamoto ya utoro kwa wanafunzi pindi wawapo hedhi.
Kilele cha maadhimisho ya siku ya mwanamke dunia uadhimishwa Machi 08 kila mwaka ambapo uambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo kutembelea wahitaji, utoaji wa zawadi, misaada kwa makundi maalum pamoja na kutoa elimu kwa jamii.