*********************
Na John Walter-Babati
Mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange amekabidhi pikipiki nane za awamu ya kwanza kwa watendaji wa kata nane za Halmashauri ya wilaya Babati zilizonunuliwa na serikali kwa ajili ya kurahisisha majukumu yao katika kata.
Mkuu wa wilaya amesema ni mapinduzi makubwa yanayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan ambapo mwaka jana katika wilaya ya Babati alikabidhi pikipiki Zaidi ya hamsini kwa maafisa ugani.
Twange amesisitiza nidhamu katika matumizi ya piki piki hizo kwa kuziendesha kwa kuzingatia taratibu zote za usalama bara barani.
Pikipiki hizo nane zilizokabidhiwa kwa watendaji leo Machi 6,2023 zimenunuliwa na serikali kupitia ofisi ya Rais TAMISEMI, fedha zilizotokana na sehemu ya kodi ya majengo inayokusanywa na hazina.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Babati Anna Mbogo, amesema wameanza kuzigawa kwenye kata nane za pembezoni ikiwemo Qash, Gidas, Duru,Secheda,Dabil, Qameyu,Magara na Nkaiti.
Mbogo amewataka watendaji hao wakazitumie pikipiki hizo katika shughuli za serikali na kuzitunza kwa kuzifanyia marekebisho ya mara kwa mara.