***********************
Na. Damian Kunambi, Njombe.
Katika kuhakikisha uvuvi wa ziwa nyasa unaimarishwa na kutoa samaki wengi kulingana na soko, Hatimaye wavuvi wa ziwa hilo wilayani Ludewa mkoani Njombe wameanza hatua za awali za ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba baada mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga kuwezesha upatikanaji wa kizimba kimoja ambacho kimegharimu kiasi cha sh. Ml. 20 kupitia mfuko wa jimbo.
Akizungumza mara baada ya kutembelea eneo hilo la kizimba mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga akiwa sambamba na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi wilaya na viongozi wa kata amesema Kizimba hicho kitakachowekwa samaki ishirini elfu tayari kimewekwa katika eneo la Chuva lililopo katika kitongoji cha Lutala kata ya Iwela ambako ndiko mradi huo utakako tekelezwa na kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwa sekta ya uvuvi na kuongeza ajira kwa vijana.
Amesema awali aliwapeleka kupata mafunzo wataalamu wa sekta ya uvuvi wa wilaya hiyo katika maeneo mbalimbali ikiwemo mkoani Mwanza na kisha kuleta kufanyiwa utafiti wa eneo linalofaa kwa uwekezaji huo ambapo eneo hilo la Chuva ndilo lililo bainika kuwa linafaa kuweka kizimba na kuzalisha samaki hao.
“Ziwa hili limekuwa likitoa samaki wachache na wadogo huku samaki walio wakubwa wakibaki ziwani, hivyo katika kipindi hiki niliona ni vyema kutenga kiasi cha sh. Ml. 20 ili kuweza kuanza na kizimba kimoja na baada ya hapo tutaendelea kuwekeza zaidi’ Amesema Kamonga.
Ameongeza kuwa kwa sasa wilaya hiyo inaelekea katika kuanza kwa miradi mikubwa kama ya Liganga na Mchuchuma hivyo kufanikiwa kwa mradi huo kutasaidia kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja, pato la halmashauri na nchi kwa ujimla hivyo vijana wanapaswa kutumia fursa ya mikopo ya Halmashauri ili kufanya uwekezaji zaidi.
Stanley Kolimba ni mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilayani humo ambaye pia ni mwenyeji wa ukanda huo wa mwambao amesema uvuvi uliopo sasa ni uvuvi usio na manufaa kwani wavuvi wanashindwa kupata samaki wakubwa huku katibu wa chama hicho ngazi ya Wilaya Gervas Ndaki amesema idadi hiyo ya samaki watakaofugwa kwa kizimba kimoja ni wengi hivyo vijana watumie fursa hiyo kwani itawasaidia kuongeza vipato.
Aidha kwa upande wa wavuvi wa ziwa hilo akiwemo Richard Kayombo wamefurahishwa na kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo huku wakimshukuru mbunge Kamonga, sambamba na kumuomba kuufanya mradi huo kuwa endelevu.