WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima,akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma kuelekea Siku ya Wanawake Duniani inayoadhimishwa Machi 08 kila Mwaka.
Na.Alex Sonna-DODOMA
IMEELEZWA Wanawake na Wasichana hawanufaiki ipasavyo na teknolojia ya kidigitali hali inayosababisha kushindwa kujikwamua Kiuchumi.
Hayo yamesemwa leo Machi 6,2023 jijini Dodoma na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuelekea Siku ya Wanawake Duniani inayoadhimishwa Machi 08 kila Mwaka.
Dk.Gwajima amesema kuwa wanawake na wasichana baadhi hawanufaiki na teknolojia ya kidigitali jambo linalowafanya kuzikosa baadhi ya fursa za kiuchumi na ajira.
“Ndugu Wanahabari, kwa ufupi, nikirejea takwimu za Dunia kwenye ripoti ya ‘UN-Secretary General’ kuhusu Kamisheni ya Hali ya Wanawake-CSW 67; inaonekana kuwa, wanawake na wasichana hawanufaiki ipasavyo na teknolojiaya kidigitali ” amesema Dk.Gwajima
Aidha ametaja vikwazo kwa wanawake kutumia mtandao kuwa ni pamoja na kushindwa kumudu gharama, kutojua kusoma na kuandika, ukosefu wa ujuzi, ukosefu wa faragha na Usalama.
Amesema katika nchi zenye uchumi wa chini asilimia 76 ya watu wake wanazo simu zinazopokea mtandao lakini asilimia 25 tu ndiyo wanatumia huo mtandao huku asilimia 52 wakiwa ni wanaume hivyo wanawake ni wachache zaidi.
Dk.Gwajima ametaja sababu nyingine wananwake kuwa nyuma kwenye matumizi ya kidigitali kuwa ni maudhui kutokidhi, kutoona umuhimu, kutomiliki simu , kutofahamu, matatizo ya upatikanaji wa nishati ya umeme, mila na desturi na vikwazo vingine.
”Mwaka 2022 takwimu zinaonesha asilimia 63 ya wanawake duniani walitumia mtandao ukilinganisha na 69 ya wanaume huku uwezo wa wanawake kumiliki simu ukiwa chini kwa asilimia 12 ukilinganisha na wanaume.”amesema
Aidha amesema Serikali kwa kushirikiana na Wadau itaendelea kuondoa vikwazo vyote vinavyokwamisha Wanawake kutumia Teknolojia na huduma za Kidigitali ili kujikwamua Kiuchumi.
“Mwaka 2020 mafunzo ya uendeshaji na ufundishaji wa TEHAMAyalitolewa kwa wakufunzi 1347 ambao wanaume 893 na wanawake 454, vilevile Serikali inawekeza katika ujenzi Barabara, Miundombinu ya Maji,Afya ,kilimo,ufugaji na Sekta zote ambapo uwekezaji huo ni nguzo kubwa katika kukuza Uchumi.”Amesema Dkt Gwajima.
Dkt Gwajima amesisitiza Wanawake kutumia Majukwaa ya uwezeshaji Kiuchumi yaliyoundwa kwenye ngazi zote katika mikoa 12 hadi sasa, ili kunufaika na fursa za Uwezeshaji zinazotolewa na Serikali pamoja na Wadau wengine.
Ameeleza kuwa maadhimisho ya siku ya Wanawake Mwaka huu nchini yatafanyika katika ngazi za Mikoa kwa kuratibiwa na viongozi wa Mikoa, ambapo kaulimbiu ni “Ubunifu na Mabadiliko ya Teknolojia:Chachu katika kufikia usawa wa Kijinsia”