Makamu Rais wa Kampuni mama ya GGML, AngloGold Ashati – anayeshughulikia miradi endelevu Ghana na Tanzania, Simon Shayo akielezea mchango wa GGML katika mdahalo wa miaka miwili ya Serikali ya awamu ya sita madarakani chini ya Rais Samia Suluhu Hassan. Mdahalo huo umefanyika juzi mjini Geita.
Mwanasheria Mkuu wa Kampuni uya Geita Gold Mining Limited (GGML) David Nzarigo (katikati) akimtambulisha Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Wayne Louw (kulia) kwa Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Safia Jongo.
NA MWANDISHI WETU
KAMPUNI ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imeeleza kuridhishwa na juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kuvutia wawekezaji na kuboresha sekta ya madini na kuifanya kampuni hiyo kuendelea kukua kila mwaka.
Pia imeahidi kuendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha lengo la mchango wa sekta ya madini kufikia asilimia 10 ya pato ghafi la Taifa linafikiwa mwaka 2025 licha ya kwamba sasa limefikia asilimia 9.2
Kauli hiyo imetolewa jana na Makamu Rais wa Kampuni mama ya GGML, AngloGold Ashati – anayeshughulikia miradi endelevu Ghana na Tanzania, Simon Shayo wakati akizungumza kwa niaba ya wadau wa sekta ya madini katika madahalo wa miaka miwili ya Rais Samia madarakani.
Shayo alitolea mfano kuwa ripoti za karibuni kutoka Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta, na Gesi Asilia (TEITI) zinaonesha GGML inachangia kati ya asilimia 30 na 40 ya mapato yote au dhahabu yote inayouzwa kwa sekta ya madini Tanzania.
“Kwetu hiyo ni faraja na hapa Geita tunaamini kwa kushirikiana na serikali ya mkoa na halmashauri yetu na wilaya zetu tunaweza kuufanya mgodi wetu ukazalisha zaidi na wakati wote mgodi uendelee kuzalisha zaidi ya wakia 500,000 kwa mwaka,” alisema.
Aidha, alisema wanaamini sekta madini inaweza kuvuka malengo yaliyowekwa na Serikali iwapo wawekezaji pamoja na wachimbaji wadogo wataendelea kujengewa mazingira bora ya uwekezaji.
“Tunaendelea kuiomba serikali chini ya uongozi wa Rais Samia kuendelea kutuwekea mazingira mazuri, tunaahidi kuongeza tija kwenye migodi yetu na sisi AngloGold Ashanti kupitia mgodi wetu wa GGML tunaamini wakati wote tutaendelea kuwa sehemu kubwa ya mafanikio hayo ya sekta ya madini,’ alisema.
Alisema uwepo wa GGML Tanzania, unajitafsiri si tu kwenye uchimbaji wa dhahabu na ulipaji wa kodi lakini kwenye uwekezaji kwenye jamii.
“Tunu yetu kubwa ni kwamba jamii ionekane kunufaika kwa sisi kuwepo hapa, tumejitahidi kwa uwezo wetu tangu tumeanza uchimbaji mjini Geita mwaka 2000 lakini tangu tumeanza kuingia makubaliano na halmashauri zetu kwa maana utekelezaji wa mpango wa CSR.
“Uwajibikaji wetu kwa jamii kupitia mpango ambao unasainiwa kwa pamoja tangu mwaka 2017, tumewekeza kila mwaka kati ya Sh bilioni 9.2. hadi 9.5 na mwaka huu tunaamini tutapata fursa ya kuunganisha mipango miwili ya mwaka 2022 na 2023 ambapo kwa wilaya ya Geita peke yake tutawekeza kiasi cha Sh bilioni 18.4,” alisema.
Alisema uwajibikaji wa GGML kwa jamii, unajitafsiri katika elimu, afya na kipato.
Aidha, alitoa ombi kwa Serikali kuendelea kuhakikisha wanachokifanya kwa jamii kinaongeza tija kusaidia serikali kupiga hatua zaidi kwenye huduma za jamii kwa wananchi wanaozunguka mgodi kunufaika.
Akizungumza katika mdahalo huo, Mkuu wa mkoa wa Geita, Martin Shigela alisema mkoa huo ndio namba moja kwa uzalishaji wa madini ya dhahabu kwani asilimia 60 ya mapato ya Taifa inatoka kwenye madini.
Alisema kwa miaka miwili iliyopita, wachimbaji wadogo na wakati wamezalisha kilo 13,000 sawa na tani 13.5 wakati migodi mikubwa kama GGML imezalisha kilo 35,000 sawa na tani 35.
“Mchango wetu katika kipindi cha miaka miwili unaonesha kuwa ardhi ya mkoa huu ina thamani ya Sh trilioni tano ambayo ni sawa na robo ya bajeti ya Taifa,’ alisema.
Alisema kwa kipindi cha miaka miwili, zaidi ya Sh bilioni 400 zimekusanywa kama mapato katika migodi inayochimba dhahabu Geita.
“Ukiangalia miaka ya nyuma hata asilimia 50 ya fedha ilikuwa haijafikiwa. Rais wetu amejenga mazingira uwekezaji, ametangaza nchi kimataifa na wawekezaji wanaweza kuja bila kuwa na hofu wala wasiwasi wowote,” alisema.