Na. Damian Kunambi, Njombe
Katika kuhakikisha jengo la bweni la wavulana katika shule ya sekondari Lugarawa iliyopo wilayani Ludewa mkoani Njombe linarejea katika hali yake ya kawaida baada ya kuungua hivi karibuni, jeshi la Polisi wilayani humo limetoa mchango wa kiasi cha sh. 200,000 ili kukamilisha baadhi ya mapungufu yaliyojitokeza baada ya maafa hayo.
Akizungumza wakati akiwasilisha mchango huo kwa Afisa elimu Sekondari Mikael Hadu, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ludewa Deogratius Massawe amesema kotokana na umuhimu wa kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii, wao kama Jeshi la Polisi wameona ni vyema kuungana na wananchi katika kutatua janga hilo na kuhakikisha bweni linajengwa kwa wakati na kuanza kutumika kama awali.
“Fedha hizi zimechangwa na askari kwa hiyari yao, na wamefanya hivyo kutokana na kuguswa na janga hili lililotokea na kwakuwa sisi polisi ni sehemu ya watoa huduma kwa jamii hivyo tukaona ni vyema nasi tukaonyesha ushiriki wetu katika janga hili”.
Kwa upande wake afisa elimu sekondari wa wilaya ya Ludewa Bw. Mikael Hadu amelishukuru jeshi la polisi wilaya ya Ludewa kwa kuungana na wadau mbalimbali wa elimu kwa kutoa mchango huo na kuahidi kuzifikisha fedha hizo katika kamati ya maafa.
Ikumbukwe kuwa bweni hilo la wavulana la shule ya Sekondari Lugarawa liliungua hivi karibuni na kuteketeza vitanda, magodoro na baadhi ya vifaa vya wanafunzi huku chanzo cha moto huo kikidhaniwa kuwa ni hitilafu ya umeme.