KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viatilifu Tanzania (TPHPA), Prof. Joseph Ndunguru,akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 1,2023 jijini Dodoma (hawapo pichani) wakati akieleza utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita.
Na.Alex Sonna-DODOMA
Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viatilifu Tanzania (TPHPA) imejipanga kuendelea kufanya ukaguzi wa viwatilifu mara kwa mara kwa watengenezaji, wasambazaji, wauzaji na watumiaji ili kupunguza athari ya kuwepo kwa viuatilifu bandia.
Hayo yameelezwa leo Machi 1,2023Jijini na Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo,Prof. Joseph Ndunguru wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo katika kipindi cha serikali ya awamu ya sita.
Prof,Ndunguru amesema bado wanakabiliwa changamoto ya viatilifu bandia kuingia nchini kupitia maeneo ya mipakani na njia za panya.
Amesema kutokana na hali hiyo wamejipanga kuendelea kufanya ukaguzi wa viwatilifu mara kwa mara kwa watengenezaji, wasambazaji, wauzaji na watumiaji ili kupunguza athari ya kuwepo kwa viuatilifu bandia.
Prof Ndunguru amesema jumla ya viuatilifu vipya 409 na kampuni za ufukizaji 198 vilisajiiliwa katika maeneo mbalimbali nchini na mamlaka imeendelea kufanyika kaguzi ili kupunguza uwepo wa viuatilifu bandia.
Amesema chunguzi za sampuli 103 za shehena za mimea zilifanyika katika maabara na vitalu nyumba ambapo jumla ya maombi 762 ya vibali vya kuingiza vipando nchini Tanzania yalipokelewa.
“Tumefanya Kaguzi 7 zilifanyika katika karantini za wazi,miwa na viazi mviringo na matunda ya Sapodilla .Vipando vyote kwenye Karantini hizo vilikidhi matakwa ya afya ya mimea ya Tanzania,”amesema Prof,Ndunguru
Prof. Ndunguru amesema mamlaka imeweza kukusanya jumla ya sampuli 400 za nasaba za mimea ya aina mbalimbali na kuhifadhi katika benki ya mbegu.
Katika kukabiliana na viwavi jeshi,Prof,Ndunguru amesema jumla ya lita 81,563 za Profenofos zimesambazwa katika Halmashauri 57 za mikoa lengo likiwa ni kudhibiti uharibifu katika mazao ya nafaka.
Ameitaja mikoa hiyo ni Lindi, Pwani, Morogoro, Tanga, Geita, Manyara, Kilimanjaro, Dodoma, Singida, Dar es salaam, Katavi na Arusha.
Prof Ndunguru amesema mamlaka imekagua tani 5,343,380.59 za mazao ya nafaka, bustani, mizizi, mbegu za mafuta katika vituo vya mipakani, bandari na viwanja vya ndege.
Amesema jumla ya vyeti 29,033 vya usafi wa mimea kwa ajili ya kuruhusu mazao kusafirishwa nje ya nchi na vyeti 3359 vya kuruhusu mazao kuingia nchini vimetolewa.
Amesema mamlaka imedhibiti ndege aina ya kwelea kwelea milioni 227.4 na kufanikiwa kuokoa tani 1056.3 za mazao ya nafaka.
Hata hivyo amesema wanakabiliwa na changamoto ya uelewa mdogo wa wakulima na wadau wengine juu ya matumizi sahihi ya viuatilifu pamoja na uwepo wa wauuzaji wa viuatilifu na mazao ya mimea wasio waaminifu.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Karantini ya Mimea ya Taifa kutoka TPHPA Dk.Benjamini Ngowi amesema kuna karantini za wazi ambazo kazi zake ni kukagua mimea inayoingizwa kama ina changamoto yoyote.
Amesema kaguzi 7 zilifanyika katika karantini za wazi za miwa na viazi mviringo na vilikidhi matakwa ya afya ya mimea ya Tanzania.
“Tumekuwa tukiwaita maafisa ugani tunawapa elimu na tunakutana na viongozi wa wakulima ili kuweka mikakati ya pamoja kukabiliana na changamoto ya wadudu waharibifu na jinsi ya kulima kisasa,”amesema Dk Ngowi.