Waziri wa ujenzi na uchukuzi, Profesa  Makame Mbarawa akipata maelezo ya mradi huo kutoka kwa Kaimu Meneja wa TBA mkoa wa Arusha ,Mhandisi Juma Dandi akiwa ziarani  mkoani Arusha.
Kaimu Meneja wa TBA mkoa wa Arusha ,Mhandisi Juma Dandi akitoa  maelezo juu ya mradi huo kwa Waziri wa ujenzi na uchukuzi alipotembelea mradi huo jijini Arusha.
Julieth Laizer ,Arusha.
Waziri wa uchukuzi na ujenzi Profesa Makame Mbarawe  leo ametembelea mradi wa  ujenzi wa wakala wa majengo Tanzania (TBA) Mkoa wa Arusha na kuridhishwa na kasi ya  ujenzi huo pamoja na thamani  halisi  ya fedha zilizotumika kuendana na mradi huo.
Hata hivyo amesema kuwa, mradi huo umefanyika kwa umakini mkubwa na fedha zilizopangwa  kutumika  katika mradi  huo zinaendana na mradi wa  jengo hilo.
Akizungumza mara baada kutembelea jengo hilo katika ziara yake mkoani Arusha,Mbarawa  amesema jengo hilo linaendana na thamani ya fedha ambazo zinatokana na mapato ya ndani ya taasisi hiyo.
Hata hivyo Waziri amesema kuwa, wamejipanga kuhakikisha wanatumia  mfumo maalumu wa kitasa janja(Smart Lock) kwenye  nyumba hizo ili kudhibiti  uwepo kwa wadaiwa  sugu  ambao wamekuwa wakisumbua  kulipa  pango  la nyumba. 
“Sasa hivi hatutaki  kusumbuana tena na wapangaji wetu ambao hawataki kulipa kwa wakati tukitumia  mfumo huo maalumu ikifika mwisho wa mwezi tunampa mteja onyo  la kulipa kwa muda wa  wiki moja tukiona hajalipa tunampa tena onyo la pili kwa muda wa siku tatu baada ya hapo asipolipa  mfumo wa smartlock unafanya kazi yake kila akitaka kuingia ndani inagoma  hadi alipie  bango la nyumba na hiyo ndio njia nzuri ya kuwabana wadaiwa sugu na kuepukana kusumbuana nao hadi mahakamani.’amesema Waziri Mbarawa.
Kwa upande wake Kaimu Meneja TBA mkoa  wa Arusha ,Mhandisi Juma Dandi amesema kuwa jengo hilo lina uwezo wa kuchukua familia  22 ambavyo ni kitega uchumi cha TBA ambapo wapangaji katika nyumba hiyo watapaswa kulipa kwa wakati kwani wanapokea hela kila mwezi.
Amesema kuwa mradi wa  jengo hilo  lenye ghorofa 10 umeshatumia kiasi cha shs  5.2 bilioni  hadi sasa ambapo mpaka kukamilika litagharimu Kiasi cha shs  5 .5 bilioni na unatarajiwa kukamilika rasmi ndani ya wiki mbili hadi tatu .
Aidha Mhandisi Juma amesema kuwa,kukamilika kwa mradi huo kutaweza kukidhi mahitaji ya makazi  kwa watumishi  wa umma na mapato ya serikali kwa ujumla na uwepo wa mradi huo umeweza  kuongeza idadi kubwa ya ajira  kwa mafundi  na wafanyakazi  wengine pamoja kuwepo kwa ununuzi  mkubwa wa vifaa vya ujenzi .