************************
Na. WAF – Dodoma
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amewakaribisha Katibu Mkuu Dkt. Seif Shekalaghe na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Grace Magembe na kuwataka kuendeleza ushirikiano ili kuboresha sekta ya Afya nchini.
Waziri Ummy ameyasema hayo leo katika hafla fupi ya kuwakaribisha makatibu wakuu hao iliyofanyika Ofisi za Wizara Mji wa Serikali, Mtumba Jijini Dodoma.
Waziri Ummy amemkaribisha Dkt. Shekalaghe kwenye menejimenti yake ya kwanza kama Katibu Mkuu na Dkt. Grace Magembe kama Naibu Katibu Mkuu mara baada ya kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha, Waziri Ummy amewataka Wakurugenzi na watumishi wote kutoa ushirikiano kwa Viongozi hao kwa lengo la kuendelea kuboresha sekta ya afya kama ambavyo Rais Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka.
“Sekta ya afya ni kubwa hivyo tushirikiane kuondoa changamoto ili wananchi wapate huduma zilizo bora na zinazostahili, tuwasimamie wataalamu wetu wa afya hili ni jukumu letu kwa pamoja,” amesema Waziri Ummy
Kwa upande wake Katibu Mkuu Dkt. Seif Shekalaghe amemshukuru Waziri Ummy kwa ukaribisho mzuri na ameahidi utumishi bora katika nafasi aliyoteuliwa ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa huduma za afya.
Naye, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Grace Magembe amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua katika nafasi hiyo na kuahidi kutoa ushirikiano katika maendeleo ya Sekta ya Afya.