Meneja miradi wa taasisi ya TPSF ,Max Rugaimukamu akizungumza katika mkutano huo jijini Arusha .
Mkurugenzi wa Jumuiko la maliasili Tanzania (TNRF) ,Zakaria Faustin akizungumza katika mkutano huo jijini Arusha.
Meneja ushirikishwaji wa sekta binafsi kutoka shirika la RTI wasimamizi wa mradi wa USAID -Tuhifadhi maliasili ,Dk Elikana Kalumanga akizungumza katika mkutano huo jijini Arusha.
***************************
Julieth Laizer ,Arusha
Arusha.Wadau mbalimbali kutoka sekta binafsi na sekta ya umma ,wamekutana jijini Arusha kuweza kujadili biashara endelevu kwenye ushoroba wa kwa kuchinjwa unaounganisha njia kati ya hifadhi ya Tarangire na Manyara .
Akizungumza katika mkutano huo jijini Arusha Meneja miradi wa Taasisi ya TPSF Max Rugaimukamu amesema kuwa, mkutano huo umeandaliwa na Taasisi ya sekta binafsi Tanzania (TPSF) kwa ufadhili wa USAID -Tuhifadhi maliasili Activity.
Amesema kuwa ,lengo la mkutano huo ni kuangalia namna ya kufanya biashara yenye uendelevu zinazojali na kuangalia mazingira ya wanyamapori pamoja na kujadili changamoto na mapendekezo ya kikodi na zisizo za kikodi sambamba na kuzungumzia maboresho katika maeneo hayo ili kuwekeza uwekezaji na biashara katika sekta ya utalii na mifugo.
Ameongeza kuwa,taasisi hiyo imekuwa ikifanya kazi katika kuleta ufahamu kwa sekta binafsi juu ya umuhimu wa ushoroba katika uhifadhi wa maliasili na ukuzaji wa uchumi .
“Unajua tunawapa mafunzo ili waweze kujua umuhimu wa kutunza ushoroba kwani endapo zitatunzwa inasaidia pia kutunza misitu,wanyamapori,na vitu vyote vilivyopo ndani ya ushoroba “amesema .
Kwa upande wake Meneja ushirikishwaji wa sekta binafsi kutoka shirika la RTI International wasimamizi wa mradi wa USAID Tuhifadhi maliasili,Dkt Elikana Kaluwanga amesema kuwa,mradi huo unatekelezwa maeneo mbalimbali nchini lengo likiwa ni kuwepo kwa usimamizi mzuri wa shoroba(mapito ya wanyamapori).
Amesema kuwa,wadau hao wa sekta ya utalii kutoka sekta binafsi na umma kwa pamoja wameweza kujadili fursa za utalii na ufugaji zilizopo katika maeneo ya ushoroba na kupata mafunzo namna ya kuweza kuendelea kutunza shoroba hizo ili ziendelee kuwepo na kutumiwa na wanyamapori kwa ajili ya kuongeza utalii zaidi .
“mradi huu unalenga kuwezesha wadau hao kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo katika usimamizi wa maliasili hasa shoroba kwani kwao ni muhimu sana kama wawekezaji wakubwa katika sekta ya utalii.”amesema.
Ameongeza kuwa , sasa hivi serikali ya Tanzania imefikia hatua ya kuyaainisha hayo maeneo ili yasipotee ambapo kwa Tanzania kuna takribani shoroba 61 ,hivyo ni jukumu lao kwa kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na wananchi kuhakikisha wanaunga mkono na kutoa kipaumbele kwenye maswala ya shoroba, huku akiomba serikali kuweka alama ili kunusuru kizazi hiki na kijacho.
Naye Mmoja wa wadau wa utalii, Mkurugenzi wa Jumuiko la maliasili Tanzania, Zakaria Faustin amesema kuwa,ni vizuri serikali ikafanya mabadiliko ya huo mwongozo wa maeneo ya mapito ya wanyama ili kuainisha matumizi mbalimbali na wananchi wawe na imani kuwa maeneo hayo hayachukuliwa na serikali bali yataendelea kuwa ya kwao.