Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wadau wa zao la Chikichi kuhusu mafanikio ya mpango mkakati wa kufufua, kupanua na kuendeleza zao la chikichi nchini, kwenye ukumbi wa NSSF, Kigoma
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Watanzania wana kila sababu ya kutembea kifua mbele na kujivunia utafiti uliofanyika hapa nchini na kupata mbegu mpya ya michikichi ambayo imeonesha mafanikio makubwa.
“Baada ya kukaa na kufanya tathmini ya zao la chikichi hapa Tanzania, na leo nimesikia michango ya wadau wote. Nimejiridhisha kwamba utafiti tulioufanya wa kuzalisha mbegu ya Tanzania ambayo inaota na kutoa matunda ndani ya miaka miwili hadi mitatu, ninayo furaha kutamka kuwa utafiti ule umefanikiwa,” alisema na kuamsha shangwe miongoni mwa wadau wa zao hilo.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana usiku (Jumapili, Februari 26, 2023) wakati akihitimisha kikao chake na wadau wa zao la chikichi mkoani Kigoma kwenye ukumbi wa NSSF. Mbegu hiyo bora ya michikichi aina ya TENERA inatoa mafuta mara tatu zaidi ya aina ya DURA ambayo inalimwa na wakulima kwa takribani asilimia 90.
Alisema mtu yeyote anayetaka kulima chikichi anaweza kufanya hivyo kwa sababu mbegu zipo. “Tulianza kuzalisha mbegu mwaka 2018 na ilipofika mwaka 2020 tukaanza kupanda miche na leo tunaona matunda yanapatikana.”
“Twendeni mashambani, tutumie miche yetu iliyozalishwa ama na taasisi zetu, Halmashauri zetu au vyama vya msingi (AMCOS). Tuna kazi ya kuhakikisha zao la chikichi linaenda kwa spidi kali zaidi.”
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametuagiza kila mkoa, kila wilaya tutenge maeneo ya kilimo lakini kuna baadhi hadi leo hii bado hamjagawa maeneo, tena vijana wapo na wanataka kulima. Inasikitisha kuona wataalamu tupo, nia ya dhati ya Serikali ipo lakini watu hamchukui maamuzi. Tunataka sasa, tutoke hapo tulipo.”
Akifafanua kuhusu umuhimu wa kuwa na mashamba makubwa ya michikichi, Waziri Mkuu alisema si lazima mashamba hayo yalimwe au kumilikiwa na mtu mmoja. “Jiungeni watu kadhaa na mtenganishe hizo ekari zenu kwa barabara lakini lazima yawe sehemu moja,” alisisitiza.
Akitoa maagizo mahsusi kabla ya kufunga kikao hicho, Waziri Mkuu alizitaka Halmashauri zinazolima zao la chikichi, ziimarishe vitalu vya miche ya zao hilo. Pia alizitaka zitoe fedha zilizokuwa zinatengwa kwa ajili ya vitalu na kuzipatia taasisi zinazozalisha miche ikiwemo TARI–Kihinga, JKT Bulombora na gereza la Kwitanga ili zizalishe miche kwa ajili ya Halmashauri husika na kisha wazisambaze bure kwa wakulima katika maeneo yao.
Alielekeza ufanyike ufuatiliaji wa karibu wa miche ya michikichi inayopelekwa kwa wakulima ili miche hiyo ikue na kufikia hatua ya kuzaa. Pia aliitaka Taasisi ya Utafiti wa Mbegu (ASA) iimarishe ushirikiano na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) ili kuzalisha miche mingi zaidi ya michikichi.
Akisisitiza kuhusu utoaji elimu, Waziri Mkuu alisema wadau wa zao la michikichi wakutanishwe mara kwa mara ili kutathmini na kujadiliana changamoto zilizopo na kuzipatia ufumbuzi. Pia alitaka waelezwe fursa zilizopo katika zao la michikichi na wananchi wataarifiwe ili waweze kutumia fursa hizo.
Aliitaka Wizara ya Kilimo iandae filamu ya Kitanzania inayoelezea vizuri kilimo cha zao hilo ili wakulima waone kwa uhalisia na kupata elimu kuhusu zao hilo.
Waziri Mkuu aliitisha kikao hicho ili kufanya tathmini ya zao la chikichi tangu Serikali ilipoanza mkakati wa kulifufua Julai, 2018. Alikutana na wadau hao ili kutafuta njia za kuliendeleza na kuhakikisha nchi inakuwa na kiasi cha kutosha cha mafuta ya mawese, hatua ambayo alisema itasaidia nchi kuepuka gharama kubwa zinazotumika kuagiza kiasi kikubwa cha mafuta kutoka nje nchi.
Kila mwaka, Serikali inatumia shilingi bilioni 470 kuagiza tani 360,000 kutoka nje ya nchi ili kufidia pengo la tani 650,000 za mafuta ya kula zinazohitajika nchini. Serikali ilichukua hatua za makusudi za kuliingiza zao la michikichi katika orodha ya mazao ya kimkakati ili kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa soko. Mazao mengine ya kimkakati ni pamba, tumbaku, kahawa, korosho, chai, mkonge, zabibu na alizeti.
Mapema, wadau mbalimbali walitoa maoni yao na kuelezea changamoto wanazokabiliana nazo ikiwemo ukosefu wa mitaji, kutokopesheka kwenye mabenki, ukosefu wa ardhi ili kufungua mashamba makubwa na ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu mikopo.
Wadau hao walijumuisha wakulima wadogo na wa kati, wazalishaji miche, wakamuaji mawese, viongozi wa vijiji, viongozi wa vyama vya ushirika, viongozi wa taasisi za fedha, viongozi wa wilaya, halmashauri na mkoa na Wabunge wa mkoa huo.