Na.Mwandishi Wetu-NJOMBE
Serikali mkoani Njombe imeingia mikataba yenye thamani ya zaidi ya bil 2.2 na makampuni matatu ya Kitanzania ya ujenzi wa miradi mitatu ya maji itakayonufaisha wakazi zaidi ya elfu 8 katika vijiji 9 vyenye changamoto kubwa ya maji wilayani Makete ambayo itatekelezwa katika kipindi cha miezi sita kuanzia sasa.
Katika mikataba hiyo iliyosainiwa mbele ya wananchi wa kijiji cha Mfumbi kilichopo mpakani mwa Mkoa wa Njombe na Mbeya ,Kampuni ya HARFRE TECH LTD imechukua kandarasi ya ujenzi wa mradi wa Usalimwani-Mfumbi wenye thamani ya mil mia 7.3,Mradi wa Ujuni-Nkenja wenye thamani ya mil mia 8.6 ukichukuliwa na kampuni ya Gold Star.Co.ltd na Kampuni ya Advanced Engineering ikiingia mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji wa Kidope -Madihani wenye thamani ya mil mia 6.3.
Akitoa malekezo kwa wakandarasi na mameneja wa RUWASA punde baada ya kusaini kandarasi za utekelezaji wa miradi hiyo na kuelezwa hali ya upatikanaji wa maji kwasasa,Mkuu wa wilaya ya Makete Juma Sweda amesema anatoa siku 14 kufanya maandalizi ya ujenzi na kisha kutoa onyo kwa ambae hatakamilisha mradi ndani ya muda uliyopangwa.
“Leo tunasaini mikataba hii nataka kuona ndani ya siku 14 wakandarasi wakitumia kuleta mitambo eneo la mradi na sitegemei kuwe na sababu nyingi za kuchelewa kutekelezwa,alisema Juma Sweda DC Makete”
Awali akisoma taarifa meneja wa RUWASA mkoa wa Njombe mhandisi Sadick Chaka amesema Katika bajeti ya 2022\23 makete imetengewa kiasi cha bil 1.65 ambapo miradi 12 ya maji inatarajiwa kutekelezwa huku katika robo ya kwanza miradi 7 imeanza kutekelezwa.
Chaka amesema wilaya ya Makete ni miongoni mwa wilaya zenye huduma kubwa ya maji ambapo imezidi hadi kiwango cha kitaifa kwa asilimia 70 na endapo miradi hiyo itakamilika kiwango cha maji kitafika asilimia 95.
“Serikali imeona ukubwa wa changamoto ya maji katika vijiji hivi ndiyo maana imeamua kutoa fedha za kutekeleza miradi hii mikubwa na leo ndiyo tunasaini mikataba,alisema meneja wa ruwasa Njombe mhandisi Sadick Chaka”
Wakati hali ya huduma ya maji kwa wilaya ya Makete ikizidi kiwango cha kitaifa ,Meneja wa Ruwasa makete Innocent Lyamuya anasema katika mradi wa maji wa Usalimwani-Mfumbi utaogharimu mil 736,762,500, Ujuni Nkenja wenye thamani ya shilingi 867,053,450 na Kidope -Madihani utaogharimu mil 634,034,700 ikikamilika itakwenda kunufaisha vijiji 9 wenye watu wasiyopungua elfu 8.
Mpaka sedema 2022 wilaya ya Makete ilikuwa imefika kiwango cha asilimia 90 cha upatikanaji wa huduma ya maji na kwamba matarajio yao ni kwamba ifikapo 2025 kiwango cha maji wilayani makete kitakuwa kimefika asilimia 100 na kisha kutoa agizo kwa mkandarasi kutumia nguvu kazi ya eneo husika kutekeleza mradi.
“Niwaombe wananchi waonyeshe ushirikiano kwa serikali na wakandarasi ili wakamilishe kazi kwa wakati ili waanze kunufaika na huduma hiyo,alisema mhandisi Innocent Lyamuya meneja wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini RUWASA Makete”.
Kwa upande wao wakandarasi waliyoingia mikataba hiyo akiwemo Haruna Ndazi kutoka Kampuni ya Harfre Tech Ltd na Cosmas Olomi kutoka kampuni ya Advanced Enginnering wanasema kabla ya kusaini mikataba walifika katika maeneo ya miradi na kujiridhisha na uwezo wao kiutekelezaji hivyo wanamatumaini ya kumakumaliza kazi katika muda uliyopangwa.
Mbali na kuridhia masharti ya mkataba wakandarasi hao wameomba serikali kutoa fedha katika wakati sahihi na wananchi kutoa ushirikiano ili kusiwepo na kikwazo cha wao kushindwa kutekeleza takwa la mikataba yao.
Nao baadhi ya wananchi akiwemo Roda Mbwilo mkazi wa Mfumbi na Daudi Yotamu kutoka Ujuni wanansema wanaishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuona ukubwa wa changamoto ya maji katika vijiji vyao na kisha kuamua kutoa fedha za kujenga miradi ya maji huku pia wakidai kwamba awali walikuwa wakilazimika kufata maji mabondeni hali ambayo ilikuwa hatari kwa akina mama na watoto.
Katika hatua ngingine wamesema kuna wakati ndoa zao zilikuwa hatarini kwasababu walipotumia muda mwingi kufata maji waume zao walidhani wapo kuchepuka kwa wanaume.