Mwenyekiti wa Tume wa Madini Profesa Idris Kikula amewataka Wachimbaji na Wafanyabiashara wa madini nchini kuzingatia Sheria, Usalama, Utunzaji wa Mazingira na Matumizi Salama ya Baruti katika uendeshaji wa shughuli za uchimbaji madini migodini, ambapo kila mchimbaji ana wajibu wa kusimamia mazingira kwa mujibu wa Sheria zilizowekwa.
Profesa Kikula ameyasema hayo leo Februari 23, 2023 kwenye ufunguzi wa mafunzo ya Usalama, Afya, Utunzaji wa Mazingira na Matumizi Salama ya Baruti kwa Wachimbaji wadogo wa madini, yaliyofanyika Mkoani Mara ambayo yamekutanisha Wakurugenzi, Mameneja, na Watumishi kutoka Tume ya Madini, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara, Viongozi wa Wachimbaji wadogo na Wachenjuaji wa Madini, pamoja na Wafanyabiashara na Wamiliki wa Migodi wa Mkoa wa Mara.
Profesa Kikula amesema kuwa mafunzo hayo ya siku mbili, yanalenga kuhakikisha kuwa shughuli za uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya madini zinafanyika kwa kuzingatia Usalama, Afya na Utunzaji wa Mazingira kwa kufuata Sheria, Kanuni na miongozo mbalimbali iliyowekwa.
Amesema kuwa mafunzo hayo yatazingatia pia utaratibu wa utoaji leseni za uchimbaji, uchenjuaji, biashara ya madini hususan kwenye usimamizi wa masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini nchini.
“Kupitia mafunzo haya naamini mna wajibu mkubwa wa kuimarisha mfumo wenu wa utendaji kazi kwa kuangalia usalama katika maeneo mnayochimba ili kuhakiksha kuwa taifa halipotezi nguvu kazi ili tuwe na uchimbaji endelevu wa kuimarisha maisha yetu na jamii inayotuzunguka,” amesema Profesa Kikula.