Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MWENYEKITI wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Kiria Ormemei Laizer amesema Mkurugenzi wa Taasisi ya ECLAT Foundation Peter Toima amefanya mambo makubwa mno kuliko mwanasiasa yeyote Simanjiro hivyo aungwe mkono.
Kiria ameyasema hayo kwenye uzinduzi wa elimu ya afya ya uzazi wa mpango kwa kina baba na ahadi ya ukarabati wa madarasa ya shule ya msingi Komola na ujenzi wa madarasa ya shule shikizi ya Olembole utakaofanywa na shirika la ECLAT Foundation.
Amesema Toima ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara, ameweka alama kubwa ya maendeleo kwenye maeneo mbalimbali nchini hususani katika wilaya ya Simanjiro.
Amesema shule mbalimbali zimejengwa na shirika la ECLAT Foundation hivyo kusababisha jamii hasa ya watoto wa kifugaji kupata elimu kwa ukaribu tofauti na awali.
“Kwenye Wilaya ya Simanjiro hakuna mwanasiasa aliyefanya mambo makubwa kwa kuwekeza kwenye miundombinu ya elimu kama mzee Toima hivyo tumuunge mkono,” amesema Kiria.
Diwani wa kata ya Komolo ambaye pia ni Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Baraka Kanunga amesema Toima ni mwana maendeleo aliyefanya makubwa.
“Mzee Toima na shirika lake la ECLAT Foundation chini ya wajerumani wa shirika la Upendo wamefanikisha maendeleo mengi Simanjiro kwa kujenga shule katika kata mbalimbali,” amesema Kanunga.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Simanjiro, Anna Shinini amesema Toima kupitia shirika la ECLAT Foundation amefanya mengi anastahili kupongezwa.
“ECLAT Foundation wamefanikisha miundombinu mbalimbali ya masomo hivyo kuinga mkono serikali katika kusaidia wanafunzi hasa wasichana kupata elimu,” amesema Shinini.
Amesema kupitia miundombinu hiyo wanafunzi wa Simanjiro wakijiendeleza kielimu kikamilifu watakuwa wataaalamu wa miaka ijayo kwenye sekta ya elimu, afya na taaluma nyingine.