Na Mwandishi wetu, Mirerani
WADAU wa madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, ambao wana leseni ambazo hazifanyi kazi wamepewa mwezi mmoja kuzitolea maelezo la sivyo zitafutwa.
Leseni hizo zinapaswa kutolewa sababu kwa nini zisifutwe na zikagawiwa kwa watu wengine wenye uhitaji, ndani ya mwezi mmoja zitolewe maelezo yake, kinyume na hapo zitaandikiwa hati ya makosa na baadaye zitafutwa.
Afisa madini mkazi wa Mirerani (RMO) mhandisi Menard Msengi ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye kikao na wachimbaji, wafanyabiashara wa madini na mameneja wa migodi.
RMO mhandisi Msengi amesema leseni zote zinazodaiwa ada ya mwaka zilipiwe mara moja kabla wamiliki wake hawajapewa hati za makosa.
“Kumekuwa na maombi mengi kwenye mfumo ambayo hayajalipiwa hivyo naelekeza maombi yote yawe yamelipiwa ndani ya siku 30 baada ya hapo maombi hayo yatafutwa,” amesema RMO mhandisi Msengi.
Amesema leseni zote za uchimbaji wa kati (MLS) ziwasilishe mpango kazi wao na mpango wa ufungaji wa mgodi.
“Kila mmiliki wa leseni anatakiwa kutekeleza masharti aliyopewa wakati anakabidhiwa leseni hiyo ikiwa ni pamoja na kuandaa tathmini ya awali ya utunzaji mazingira (EPP) na awasilishe kiapo cha uadilifu,” amesema.
Ameelekeza wachimbaji wote wawe wanaingia mikataba yenye tija na wafadhili, ili kuepusha migogoro ya mara kwa mara na mikataba hiyo lazima isajiliwe na ofisi ya RMO.
“Naelekeza mtu yeyote asiyekuwa na leseni ya broker asijihusishe kabisa na biashara ya kununua madini, madini yote yaletwe soko la madini hapa Mirerani,” amesema RMO mhandisi Msengi.
Hata hivyo, wadau hao wa madini Mirerani, walielezewa mada mbalimbali ikiwemo taratibu za matumizi na utunzaji sahihi wa baruti, usalama na afya katika maeneo ya uchimbaji na utunzaji na uhifadhi mazingira katika maeneo ya uchimbaji.
Pia walielezewa juu ya ulipaji wa tozo mbalimbali za Serikali na utunzaji wa kumbukumbu na udhibiti wa madini katika migodi na taratibu za utoaji wa taarifa za uzalishaji.