Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akipokea zawadi kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Bibi. Nyakaho Mahemba leo Februari 23, 2023 jijini Dar es Salaam ikiwa ni mara ya kwanza tangu ateuliwe kuongoza wizara hiyo hivi karibuni.
Na Shamimu Nyaki
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amewasisitiza wadau wa Utamaduni na Sanaa ambao wamenufaika na ambao watanufaika na mikopo inayotolewa na Mfuko wa Utamaduni na Sanaa kurejesha mikopo hiyo kulingana na makubaliano.
Mhe. Pindi Chana ametoa agizo hilo Februari 23, 2023 alipofanya ziara katika Ofisi za mfuko huo tangu ateuliwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuongoza wizara hiyo.
“Namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuridhia fedha kwa ajili ya mfuko huu ambao una lengo la kusaidia wadau wetu, nitoe rai kwenu wadau kutumia fedha hizo kwa ajili ya kazi zinazokusudiwa ili muendeleze kazi zenu,” Mhe. Pindi Chana.
Amewataka wadau wa Sanaa na Utamaduni kutumia fursa za mikopo inayotolewa na Taasisi mbalimbali za kifedha ikiwemo mikopo ya Halmashauri ili kuboresha kazi zao.
Aidha, amemuagiza Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo Nyakaho M.Mahemba kuongeza uwezo wa kutafuta fedha kwa kushirikiana na Tasisi nyingine za fedha ili Wasanii wengi zaidi waweze kunufaika.
Awali akiwasilisha taarifa ya Mfuko, Afisa Mtendaji Bi. Nyakaho M.Mahemba amesema Mfuko huo tayari umetumia takriban Shilingi bilioni 1 katika kutoa mikopo kwa Wasanii.