KATIBU Mtendaji Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Prof.Charles Kihampa,akizungumzana waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Februari 22,2023 jijini Dodoma wakati akielezea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za tume hiyo kwa kipindi Cha miaka miwili ya uongozi wa Serikali ya awamu ya 6.
Na.Alex Sonna-DODOMA
KATIBU Mtendaji Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Prof.Charles Kihampa,amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 serikali imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 6.4 kupitia Elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi kwa ajili ya kuimarisha uthibiti ubora na uhuishaji wa mitaala ya vyuo vikuu.
Hayo ameyasema leo Februari 22,2023 jijini Dodomawakati akielezea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Time ya Vyuo Vikuu Tanzania kwa kipindi Cha miaka miwili ya uongozi wa Serikali ya awamu ya 6.
Prof.Kihampa amesema kuwa lengo ni kuhakikisha elimu itolewayo na vyuo vikuu Tanzania ina kidhi kiwango cha ubora kitaifa ,kikanda na kimataifa.
“Katika kufanikisha hilo TCU imeendelea kuandaa na kuratibu mafunzo ya kubadilishana uzoefu kwa viongozi na wanataaluma wa vyuo vikuu kuhusiana na uendeshaji wa Vyuo Vikuu utengenezaji mitaala inayozingatia ujuzi na inayoendana na soko,mbinu za ufundishaji kwa wahadhiri ambao hawakusoma fani za ualimu,ulinganifu wa programu za masomi(programme benchmarks),uthibiti ubora na utengenezaji na utumiaji wa mifumo ya komputa,”amesema Prof.Kihampa
Aidha Prof.Kihampa amesema Tanzania imeendelea kuwa Taifa la watu wenye maarifa ,ujuzi,weledi na uwezo wa kutatua changamoto za kijamii na uchumi kwa manufaa ya wananchi wake ifikapo mwaka 2025 pamoja na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati unaochochewa na uwepo wa viwanda.
“Katika kuhakiki ubora TCU imeimarisha mifumo yake ya ushauri na ukaguzi wa mara kwa mara wa kawaida na wa kushtukiza Kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo kwa lengo la kuhakikisha kuwa elimu itolewayo na vyuo vikuu hapa Nchini inakidhi viwango vya ubora kitaifa,kikanda na kimataifa,
Kwa mfano katika kipindi Cha julai 2021 hadi Februari 2023 vyuo vikuu vyote 47 vilivyopo vimekaguliwa na kupewa ushauri wa maeneo yanayohitaji kuboresha,”amesema
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ni Taasisi ya Serikali, iliyoundwa mwaka 2005 kwa Sheria ya Vyuo Vikuu, Sura ya 346 ya Sheria za Tanzania. TCU ilitokana na maboresho yaliyofanywa na Serikali kwa lililokuwa Baraza la Ithibati la Elimu ya Juu (HEAC) lililoanzishwa mwaka 1995 kwa Sheria ya Elimu Sura ya 523 ya Sheria za Tanzania.