Na.Mwandishi Wetu-NJOMBE
Kufuatia kuongeza kwa migogoro katika jamii hususani ya ardhi,mirathi na ndoa ,Chama cha cha mapinduzi wilayani Njombe kimekuja na mbinu mpya ya kufatilia kiwango cha uaminifu na utendaji wa wenyeviti wa serikali za vijiji,mitaa na kata kwa kutuma kwa siri baadhi ya wafuasi wa vyama vya upinzani kuhoji serikali hizo lengo likiwa ni kujua kwa kiasi gani zinatekeleza majukumu yao katika utatuzi wa kero za wananchi.
Hayo yamebainishwa na katibu wa siasa na uenezi wilaya ya Njombe Hitra Msola katika mkutano wa chama kata ya Makambako ambapo amesema kwakuwa idadi kubwa ya viongozi wa serikali za vijiji na mitaa wanatoka kwenye chama cha mapinduzi kwasasa ,katika kuhakikisha mvuto wa chama unaongezeka kwa wananchi amelazimika kutuma watu kutoka vyama vya itikadi tofauti na wao kuhoji masuala mabalimbali yanayofanyika katika serikali za mitaa na vijiji na kisha kuwawajibisha viongozi wanaoshindwa kutatua kero za wananchi.
“Nilishatuma wafuasi Cha chadema kwenda kuhoji kwa Wenyeviti wangu wa ccm kuhusu changamoto na masuala mbalimbali ili nione uwajibikaji wao na nikapata mrejesho,niwaombe fanyeni kazi za kuhudumia wananchi,alisema Hitra Msola katibu wa siasa na uenezi CCM wilaya ya Njombe”
Katika hatua nyingine Katibu huyo wa siasa na uenezi ameweka bayana hisia zake kwa kitendo cha mkuu wa wilaya ya Njombe Kissa Gwakisa Kasongwa kulala vijijini akitatua kero za wananchi ambapo amesema katika Mji wa Makambako serikali iko mbioni kutatua kero ya maji ambayo imekuwa tatizo la muda mrefu kwa kujenga mradi wenye thamani ya bil 42 kwa ufadhili wa India Jambo ambalo litamtua mama ndoo kichwani.
“Tumepata mkuu wa wilaya jembe kwasababu amekuwa akipiga kazi usiku na mchana na wakati mwingine kulala vijijini hivyo viongozi wa CCM na Wenyeviti wa serikali za mitaa na vijiji katika wilaya hii hakikisheni mnapiga kazi ili ifikapo muda wa uchaguzi tusipate shida ya kushawishi watu watuchague,alisema Hitra Msola “
Kuhusu adha ya maji na huduma nyingine Diwani wa Kata ya Makambako John Ngimbuchi amesema licha serikali kuwa mbioni kuanza ujenzi wa mradi wa miji 28 mjini Makambako lakini serikali imeona ukubwa wa tatizo la maji Makambako na kisha kuamua kujenga mradi wa visima wa zaidi ya mil 100 katika mtaa wa Magongo.