Na Victor Masangu,Kibaha
Baadhi ya shule za msingi zilizopo katika kata ya Tumbi halmashauri ya Kibaha mji bado zinakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo kuwepo kwa uhaba wa madawati.
Katika kuliona hilo Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka ameamua kutekeleza ilani ya chama kwa kuamua kukivalia njuga suala hilo kwa kuweka mikakati ya kutoa madawati ambayo yatawasaidia wanafunzi kuondokana na adha ya kukaa kwa mlundikano.
Koka alisema kwamba lengo lake kubwa ni kuunga mkono juhudi za Rais wa awamu ya sita Mama Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya elimu ili wanafunzi waweze kusoma katika mazingira rafiki.
Pia alisema kuwa atahakikisha anatumia fedha za mfuko wa jimbo kwa lengo la kuweza kuwema miundombinu rafiki ambayo itawafanya wanafunzi waweze kusoma katika maeneo mazuri ili kuongeza kiwango cha ufaulu.
“Katika Jimbo langu la Kibaha mjini Kuna baadhi ya shule ambazo zinachsngamoto ya uhaba wa madawati na Mimi katika Jambo hilo nitalivalia njuga kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo katika kuboresha elimu,”alisema Koka.
Pia aliongeza kuwa mfuko wa jimbo umeshatoa kiasi cha shilingi milioni 30 kwa ajili ya kuhakikisha shule zinapatiwa madawati ili wanafunzi wasome katika hali nzuri bila kero zozote.
Kadhalika alisema ataendelea kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili wananchi wa kata ya Tumbi ili kuwaletea huduma mbali mbali za kijamii ikiwemo afya,elimu,maji,umeme pamoja na miundombinu ya barabara.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa cha Cha mapinduzi (CCM) Fatma Nyamka amewataka wanachama kuhahakikisha wanakuwa na umoja ili kukijenga chama na kuachana na tabia ya kuwa na makundi.
Kamati ya siasa ya chama Cha mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha mjini inaendelea na ziara yake kwa ajili ya kuongea na wanachama wake kwa lengo lla kukiimarisha chama hicho.