Mkurugenzi wa utawala na usimamizi wa rasilimali watu ,Michael John akizungumza kwenye mkutano huo .
Mkurugenzi wa idara ya utawala na usimamizi wa rasilimali watu kutoka wizara ya habari mawasiliano na teknolojia ya habari,Teddy Njau akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo.
Mkurugenzi wa bima za maisha kutoka NIC ,Hardbert Polepole akizungumza jijini Arusha leo
*****************************
Julieth Laizer,Arusha.
Arusha.Shirika la bima la Taifa (NIC) limetoa mafunzo kwa wakurugenzi wa utawala na usimamizi wa rasilimali watu kutoka wizara mbalimbali kuhusu huduma na ubora wa bima zinazotolewa na shirika hilo ili kufikisha elimu hiyo kwa watumishi wa umma na kuweza kufaidika na huduma hizo.
Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Mkurugenzi wa idara ya utawala na usimamizi wa rasilimali watu,kutoka wizara ya habari mawasiliano na teknolojia ya habari, Teddy Njau wakati akizungumza kwenye mkutano huo uliowashirikisha wakurugenzi wa utawala na usimamizi wa rasilimali watu kutoka wizara mbalimbali .
Amesema kuwa ,lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uelewa wakurugenzi hao namna shirika linavyofanya shughuli zake na maboresho mbalimbali ili kuweza kueneza elimu hiyo kwa watu mbalimbali na kuweza kutumia huduma za shirika hilo.
“Shirika limeweka mikakati mbalimbali katika kuhakikisha wameboresha huduma mbalimbali za bima zinazotolewa na shirika hilo ikiwemo kufanya vizuri sana kwenye swala la bima za maisha ambalo ni muhimu sana kwa kila mmoja wetu kuwa nalo.”amesema .
Njau amesema kuwa,kupitia mafunzo hayo watakuwa mabalozi wazuri kuhakikisha wananchi wanajiunga na bima mbalimbali kwani kwa sasa hivi huduma zimeboreshwa kwani malipo zamani yalikuwa yanafanyika sio chini ya miezi miwili ila kwa sasa hivi ndani ya siku saba tu wanapata malipo yao.
Naye Mkurugenzi wa bima za maisha kutoka shirika la bima la Taifa, Hardbert Polepole amesema kuwa, kitendo cha wakurugenzi hao kupatiwa mafunzo hayo ni ili kuweza kuwafikia watanzania wengi kwa kuwapatia elimu ya bima mbalimbali zinazotolewa na kuweza kuona fursa na umuhimu wa bima ili waelewe kwa wepesi.
Amesema kuwa, wakurugenzi wana watu chini yao na hao watu chini yao wanahitaji huduma ya bima kama mtu mmoja mmoja ili waweze kuwakatia bima na kuwaelimisha watu lazima waelewe vizuri ili kutatua changamoto za watu ambao wapo kwenye bima na kuonyesha fursa za kibima ambazo wanaweza kuzitumia.
“Serikali inataka kuongeza uchukuaji wa bima kutoka asilimia 5 iliyopo kwa sasa hadi asilimia 50 kufikia mwaka 2030 hivyo ni lazima tuhakikishe wananchi wanakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu bima ili wengi wao waweze kuitumia kwa wingi na kufikia malengo hayo.”amesema .
Amesema kuwa ,changamoto kubwa iliyopo ni elimu kwenye swala la bima watanzania wengi wanachukua bima nyingi kwa sababu ya sheria na bima nyingi ni za magari maana wengi wanaogopa kukamatwa na askari,hivyo elimu zaidi inaendelea kutolewa ili waweze kuitumia bima ya maisha ambayo ina faida kubwa kwa maisha ya baadaye.
“Hii bima ya maisha inamsaidia mtu mmoja mmoja kupata huduma ya kifedha endapo mtegemezi atafariki au kupata kilema cha kudumu ni kilio cha serikali cha muda mrefu kuona watu wanakuwa na uhakika wa kulea familia zao .”amesema Polepole.
Naye Mmoja wa washiriki ,ambaye ni Mkurugenzi wa utawala na usimamizi wa rasilimali watu,Michael John amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu sana kwani wao ndio watumishi wako chini yao ndio maana wameona umuhimu wa kuwafikishia elimu ya bima kwa wakurugenzi ili wakielewa wao wawe sehemu ya kuelimisha watumishi kuhusu umuhimu wa kuwa na bima mbalimbali.
Amesema kuwa ni muhimu sana kwani swala la bima kwa watanzania na watumishi wa bima halieweki vizuri hivyo kupitia elimu hiyo watakuwa mabalozi wazuri wa kufikisha ujumbe kwa wananchi .