NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
KAMPUNI ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania itaendela kuboresha huduma zake na kuzifanya kuwa jumuishi kwa makundi yote ya wateja ikiwa ni pamoja na uboreshwaji wa miundombinu kwa watumiaji wa viti vya magurudumu pamoja na kuweka watoa huduma kupitia lugha ya alama kwenye vituo vya kutolea huduma nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kwenye kikao kilichowakutanisha wateja wenye changamoto ya kusikia kwa lengo la kukusanya maoni ya jinsi ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja hao, Mkurugenzi wa huduma kwa wateja kutoka kampuni hiyo, Harriet Rwakatale ameweka wazi kuwa Vodacom imeendelea kuzingatia wateja wote kwa usawa ikiwemo watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali
Ameongeza kuwa Vodacom imetambua mapungufu yaliyopo kwenye utoaji huduma kwenye maduka yake ikiwemo kukosa uelewa kwa watoa huduma wake na vilevile mifumo ya bidhaa kushindwa kuwafikia watu wenye ulemavu kiurahisi hivyo imedhamiria kuboresha na kurahisisha huduma zake kwa kuanzisha huduma maalumu kwa wateja wenye ulemavu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Biashara na Masoko wa Vodacom Linda Riwa amesema wataendelea kujikita zaidi kuhakikisha kuwa bidhaa na huduma za vidacom zinatoa ujumuishi wa wateja wote lakini vilevile kutoa elimu kwa watumishi na watoa huduma wao ili kuweza kutoa huduma bora kwa wateja wenye changamoto mbalimbali
Naye Mkurugenzi wa Kituo cha Sanaa na Utamaduni Kwa Viziwi Tanzania (KISUVITA) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Mkoa wa Dar es salaam Habibu Mrope amesema huduma hizo zitasaidia kurahisisha mawasiliano kwa walemavu nchini na kuwataka makampuni mengine kuunga mkono juhudi hizo ili kuifukia Tanzania nzima
Kampuni hiyo imezindua programu ya sauti pass ambapo itamsaidia mteja mwenye changamoto kutumia simu kutumia akaunti yake ya Mpesa kupitia sauti na vilevile wametambulisha namba maalumu ya whatsapp ambapo itawawezesha wateja wenye ulemavu wa kusikia kupata huduma kupitia huduma ya lugha ya alama kupitia simu ya video.