Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati, John Mwanja akizungumza leo Februari 14,2023 wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wajasiriamali wa kata za Ikungi na Unyahati wilayani Ikungi mkoani Singida. Kutoka kulia ni Afisa Masoko na Utafiti Veta Kanda ya Kati, Sadan Komungoma na Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Ikungi, Haika Masawe. …………………………………………………… Na Dotto Mwaibale, Ikungi MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Kati imeanza kutoa mafunzo ya ufugaji wa kuku kisasa kwa wajasiriamali ili kuwawezesha wananchi kuondokane na ufugaji wa mazoea kwenda ufugaji wenye tija utakaowakwamue kiuchumi. Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kati, John Mwanja akizungumza leo Februari 14,2023 wakati wa mafunzo hayo kwa wajasiriamali wa kata za Ikungi na Unyahati wilayani Ikungi mkoani Singida ili kuwawezesha wananchi kufanya ufugaji wenye tija utakaowaongezea kipato. “Mafunzo haya ambayo ni ya kwanza kutolewa katika Chuo cha VETA Ikungi tangu kilipozinduliwa mwaka jana yanalenga kuboresha biashara za wananchi ili wafuge kuku kwa ubora ambao utaongeza thamani ya nyama na mayai,” alisema. Naye Afisa Masoko na Utafiti VETA Kanda ya Kati, Sadan Komungoma,alisema VETA imeanza kutoa kozi ambayo inahusiana na ufugaji wa kuku kutokana na Mkoa wa Singida kusifika kwa ufugaji wa kuku na kilimo cha alizeti ambao unafanyika lakini sio kwa tija hivyo VETA inawaongezea ujuzi na maarifa wananchi katika ufugaji. Alisema mafunzo haya ya muda mfupi yanatolewa kwa wajasiriamali kwenye mikoa ya kanda ya kati ambayo ni Dodoma,Singida na Manyara ili kuwawezesha wananchi kunufaika na uwepo wa vyuo vya VETA vilivyoanzishwa kila wilaya ili wajikwamue kiuchumi kupitia ujasiriamali. Naye ya Afisa Maendeleo ya Jamii Wila ya Ikungi, Haika Masawe, alisema ifike wakati wananchi wabadilike kwa kuachana na ufugaji wa mazoea na badala yake wafuge kibiashara. Haika ambaye alikuwa akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi,Justice Kijazi, alisema VETA pamoja na kutoa mafunzo haya wasaidie kuwatafutia masoko wajasiriamali. Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi imekuwa ikiwawezesha kiuchumi kwa kuwapatia mikopo ambapo hivi karibuni ilitoa mikopo ya Sh.milioni 141 kwa vikundi mbalimbali vinavyojishughulisha na ujasiriamali. Baadhi ya washiriki wamafunzo hayo akiwepo Fatma Said na Hadija Nassoro walisema mafunzo hayo yatawaongezea maarifa na mbigu za ufugaji wa kuku na kukuza uchumi wao kutokana na kuuza mayai na nyama ya kuku ambapo walitumia nafasi hiyo kupongeza Veta kwa kuwapa mafunzo hayo ambayo ni muhimu kwao |
Afisa Masoko na Utafiti Veta Kanda ya Kati, Sadan Komungoma akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo. |
Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Ikungi, Haika Masawe, akizungumza kwenye ufunguzi huo.