Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian wa Tabora akizungumza na wakulima wa zao la Tambaku wilayani Sikonge mkoani hapa .
Mkuu wa wilaya Simon Chacha akizungumza neno juu ya zao la Tumbaku mbele ya wakulima zao hilo wilayani humo.
Mwenyekiti wa chama cha kikuu cha ushirika wa zao la Tumbaku (WETCU) Hamza Kitunga akisistiza jambo mbele wa wakulima wa zao hilo.
Meneja mkuu wa Wetcu ltd,Samwel Jokea akitoa maelezo mbalimbali juu ya wakulima wa zao la Tumbaku .
mmoja ya shamba liloathiriwa na Mvua kubwa ya upepo iliyoambatana na mawe na mkulima huyo kupata hasara kubwa .
Wakulima wa chama cha msingi Makonge wilayani Sikonge wakimsikiliza mkuu wa mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Burian.
Na Lucas Raphael,Tabora
Mvua kubwa ya upepo iliyoambatana na mawe imeharibu zaidi ya ekari 15 kati ya 75 za zao la Tumbaku zilizolimwa na kusababisha hasara kubwa kwa baadhi ya wakulima wa Chama cha Msingi cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Ngulu, kilichopo kata ya Chabutwa, kijiji cha kipanga Wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora.
Wakizungumzia tukio hilo kwa masikitiko makubwa mbele ya Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian baadhi ya wakulima ambao mashamba yao yameharibiwa vibaya na mvua hiyo walieleza kuwa wamepata hasara kubwa.
Mshara Kitoli, mkulima mkazi wa kijiji hicho alisema alikuwa amelima ekari 7 za zao hilo na alitarajia kuvuna zaidi ya kilo 500 lakini mvua hiyo imemharibia mipango yake baada ya ekari 4 kuharibiwa vibaya.
Mhanga mwingine Samson Brighton, mkulima mkazi wa kijiji hicho alisema kati ya ekari 5 alizolima msimu huu ekari 4.5 zimeharibiwa vibaya na majani yote ya mmea huo yametobolewa na kuangushwa chini.
Alimweleza Mkuu wa Mkoa kuwa wana majonzi makubwa, kwa kuwa walitarajia kupata kilo nyingi msimu huu kutokana na maandalizi mazuri ya mashamba yao, kulima kwa wakati na kupata mvua za kutosha, lakini sasa furaha yao imegeuka kuwa huzuni.
Mwenyekiti wa Chama Msingi Ngulu (Ngulu Amcos) kilichoko katika kijiji hicho Gile Cheja, alisema mvua hizo zimeathiri AMCOS hiyo kwa kiasi kikubwa sana kwani walilima jumla ya ekari 75 za zao hilo lakini ekari 15 zimeharibiwa vibaya.
‘Tumepata hasara kubwa kwa uharibifu huu, sijui itakuwaje, tunaomba serikali iangalie namna ya kutusaidia, tuna mikataba na tulishapewa makisio ya kilo zinazotakiwa kuzalishwa’, alisema.
Baada ya kutembelea kijiji hicho na kujionea uharibifu uliotokea, Mkuu wa Mkoa, Balozi Batida aliaahidi kuwasiliana na Mamlaka husika ya maafa ili kuangalia namna ya kuwasaidia.
Aidha alielekeza Bodi ya Tumbaku, Chama Kikuu cha Ushirika wa wakulima wa tumbaku Mkoani hapa (WETCU LTD) na Afisa Ushirika kukaa na wahanga ili kuangalia namna ya kuokoa tumbaku iliyobaki.
Katika ziara hiyo Balozi Batilda pia alitembelea wakulima wa kijiji cha Iyombakuzova katika kata ya Misheni na kujionea jinsi tumbaku ilivyostawi vizuri baada ya kutumia mbolea ya ruzuku iliyotolewa na serikali msimu huu.
Alipongeza juhudi kubwa zilizofanywa na serikali ya awamu ya 6 kwa kuanzisha utaratibu wa kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima kwa kuwa itawasaidia kuboresha shughuli zao, kuongeza uzalishaji na kuongeza mapato yao.
Aliwahakikishia kuwa serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan inajali sana wananchi hivyo itaendelea kuweka utaratibu mzuri wa upatikanaji pembejeo hizo ili kumaliza changamoto zilizopo..