Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
WALIMU na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Tumbi ,Kibaha Mkoani Pwani wamemshukuru Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Philip Mpango kwa kutoa Sh.milioni 50 kwa ajili ya motisha kwa walimu hao.
Dkt.Mpango ametoa motisha wiki iliyopita kwenye ziara yake shuleni hapo baada ya kusomewa matokeo ya mwaka 2022,ambapo pia shule hiyo imeweka rekodi ya ufaulu kwa miaka Saba mfululizo.
Wakifanya hafla fupi kutoa shukran kwa dkt.Mpango, Mkuu wa Shule hiyo Fidelis Haule ameeleza tayari wamezindua mpango maalum na mkakati wa shule lengo ni kuhakikisha ufaulu unaishia daraja la pili ili kusudi kuendelea kumtia moyo Makamu wa Rais na Serikali .
Aidha,Haule ameipongeza Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuisaidia Shule hiyo kwani wamepokea kiasi cha Sh.milioni 200 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya Shule yake.
Amesema,tangu shule hiyo ianzishwe miaka 24 iliyopita haijawahi kufanyiwa ukarabati wowote jambo ambalo lilisababisha miundombinu kuwa mibovu na sasa kazi inaendelea na fedha hizo zinatumika katika ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara,madarasa 16,vyoo, barabara na, miundombinu ya maji.
Mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule hiyo Neema Shuma, ameeleza hatua ya kuboreshwa Shule hiyo itasaidia wanafunzi kusoma katika mazingira bora.
Matokeo ya ufaulu ya wanafunzi mwaka 2022 katika shule ya Sekondari Tumbi,daraja la kwanza waliofaulu ni 40,daraja la pili (46),daraja la tatu(31),daraja la nne(36) na waliopata 0(3) hali ambayo ilimfurahisha Dkt.Mpango na hatimaye kutoa motisha hiyo kwa walimu.