Mkurugenzi mtendaji wa Msama Promotions Alex Msama alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) ofisini kwake ambapo amemshukuru Rais Samia kutoa mikopo kwa Wasanii.
Emanuel Mabisa mwenye shati Jeupe akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu maadalizi ya tamasha la pasaka litakalofanyika tarehe 9 mwezi wa 4 2023.
*************************
Mkurugenzi wa kampuni ya Msama Promotions amempongeza Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwakumbuka na kuwajali wasanii hapa nchini kwa kuwapatia mikopo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Alex Msama amesema hatua ya Rais Samia kutoa mikopo hiyo kupitia wizara ya Utamaduni,sanaa na michezo kwa wasanii hapa nchini ni ishara tosha kuwa serikali inayajali makundi mbalimbali kwenye jamii wakiwemo wasanii
Bw Msama amemshukuru rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwakumbuka wasanii hao na kuwapa mikopo ili kuendeleza gurudumu la sanaa hapa nchini katika viwango vya juu.
Amesema hatua hiyo ya serikali itasaidia kwa kiwango kikubwa kukuza sanaa hapa nchini huku akiwashauri wasanii hao waliopewa mikopo waitumie kama ilivyokusudiwa katika maombi yao ya mikopo ikiwemo kufanya mambo ya maendeleo na kuinua uchumi wao kupitia sanaa si kununua magari ya kifahari na kuonyeshana ufahari mitaani kwani fedha hizo wanatakiwa kuzirejesha ili wasanii wengine nao waweze kupata mikopo hiyo.
“Sisi kama msama Promotions ambao ni waandaaji wa tamasha la pasaka tunaleta shukrani zetu za dhati kwa Rais Dkt Samia kwa kuwakumbuka wasanii na tunamshukuru Mungu ametupa rais mwenye upendo wa hali ya juu kwa watanzania hasa mikopo aliyotoa kwa wasanii wote wakiwemo wa bongo fleva,muziki wa bendi na Injili kwa lengo la kukuza sanaa hapa nchini”amesema Bw Msama.
Aidha amesema mikopo hiyo imeonyesha ni jinsi gani Rais Samia ana upendo mkubwa kwa watanzania wote wakiwemo wasanii huku akimpongeza waziri wa Utamaduni,sanaa na michezo Mohammed Mchengerwa kwa kuisimamia vyema wizara hiyo na mikopo ambayo imetolewa na inaendelea kutolewa kwa wasanii.
Kuhusu maandalizi ya tamasha la pasaka kwa mwaka huu mjumbe wa kamati ya maandalizi ya tamasha hilo Emmanuel Mabisa tayari wameshazungumza na waimbaji kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Kenya,Uganda,Afrika Kusini,Congo,Rwanda pamoja na Uingereza hivyo kuanzia wiki ijayo wasanii hao wataanza kutajwa kuelekea katika tamasha hilo kubwa na la kihistoria hapa nchini.
Amesema kuwa tamasha hilo linatarajiwa kufanyika Aprili 9 mwaka huu jijini Dar es salaam ambapo wasanii mbalimbali wa kitaifa na kimataifa watatoa burudani katika tamasha hilo.