Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Huduma za Meli Nchini (MSCL) akizungumza kwenye hafla ya ushushwaji wa Meli ya Mv Mwanza hapa kazi tu kwenye maji
Meli ya Mv Mwanza hapa kazi tu ikiwa tayari imeshashushwa kwenye maji katika Bandari ya Mwanza Kusini kwaajili ya kuendelea na ukamilishwaji
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Atupele Mwakibete akibonyeza kitufe ikiwa ni ishara ya Meli ya Mv Mwanza hapa kazi tu kushushwa majini
******************************
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Kujengwa kwa Meli ya Mv Mwanza hapa kazi tu itasaidia kufungua masoko mapya ndani na nje ya nchi kwakuanzisha safari mpya zitakazosaidia kurahisisha shughuli za kibiashara, kikazi, utalii na safari binafisi kweye maeneo mengi zaidi.
Hayo yamebainishwa leo Jumapili Feburuari 12, 2023 na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Atupele Mwakibete, wakati wa hafla ya kuishusha Meli hiyo kwenye maji iliyofanyika katika Bandari ya Mwanza Kusini.
Amesema Serikali iliamua kujenga Meli kubwa ili kukidhi mahitaji ya soko ambayo yanatarajiwa kuongezeka hasa pale mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza utakapokamilka.
Mwakibete ameeleza kuwa katika mwaka huu wa fedha Serikali imeendelea kutenga fedha kwaajili ya utekelezaji wa miradi mingine ya ujenzi wa Meli mpya,ukarabati wa Meli zilizopo na Chelezo katika ziwa Tanganyika na Victoria kwa lengo la kuendelea kuboresha usafiri huu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) Eric Hamissi, amesema Meli itakuwa na Madaraja sita daraja la kwanza ni VVIP kwaajili ya viongozi wa Serikali wa ngazi za juu ambao ni wanne, la pili ni VIP ambalo litabeba watu nane, la tatu ni dalaja la kwanza litabeba watu sitini, la nne ni la biashara litabeba abiria 100 la tano ni dalaja la pili ambalo litabeba abiria 200 na la sita ni daraja la uchumi ambalo litabeba abiria 800.
Amesema Meli hiyo hadi sasa inauzito wa tani 3000 na hadi kukamilika itakuwa na uzito wa Tani 3500,urefu mita 92.6 na itakuwa na uwezo wa kusafiri umbali mrefu kutokana na injini zake kuwa na uwezo mkubwa.
Awali akizungumza kwenye hafla hiyo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima, amesema usafiri wa njia ya maji ni tegemeo kubwa sana kwa wakazi wa Mikoa inayopakana na Kanda ya ziwa hivyo kukamilika kwa Meli hiyo utasaidia kuchochea maendeleo ya wananchi na uchumi wa Taifa kwa ujumla.