Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Pwani Bi.Savera Salvatory akizungumza katika ufungaji wa hafla ya kutembelea mradi wa Afya Tek na Usimamizi Shirikishi juu ya Masuala ya Afya katika halmashauri na Manispaa ya Kibaha .
Kiongozi wa Mradi wa Afya –Tek Dkt.Angel Dillip ikiwa ni katika hafla ya majumuisho mara baada ya kutembelea mradi wa Afya Tek na Usimamizi Shirikishi juu ya Masuala ya Afya katika halmashauri na Manispaa ya Kibaha.
Afisa Ufuatiiaji na Tathmini Elimu ya Afya kwa Umma ,Idara ya Kinga ,Wizara ya Afya Erick Msunyaro akiwasilisha taarifa ya majumuisho ya matembezi ya Miradi ya Afya Tek Halmashauri ya Kibaha pamoja na Manispaa ya Kibaha Mkoani Pwani.
Mtaalam Mshauri wa Afya ya Mama na Mtoto kutoka shirika lisilo la kiserikali la Apotheker kupitia Mradi wa Afya Tek Dkt.Suleiman Kimata akiteta Jambo katika katika hafla ya majumuisho mara baada ya kutembelea mradi wa Afya Tek na Usimamizi Shirikishi juu ya Masuala ya Afya katika halmashauri na Manispaa ya Kibaha.
Picha ya washiriki mbalimbali katika hafla ya majumuisho mara baada ya kutembelea mradi wa Afya Tek na Usimamizi Shirikishi juu ya Masuala ya Afya katika halmashauri na Manispaa ya Kibaha.
Washiriki mbalimbali wakiwemo wawakilishi kutoka Wizara ya Afya,Baraza la Famasi Tanzania,watumishi wa Afya -Tek ,Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Ofisi ya Katibu Tawala pamoja na watumishi wengine sekta ya Afya kwa Ujumla wakiwa katika picha ya Pamoja katika hafla ya majumuisho mara baada ya kutembelea mradi wa Afya Tek na Usimamizi Shirikishi juu ya Masuala ya Afya katika halmashauri na Manispaa ya Kibaha.
…………………………
Na.Faustine Gimu,Elimu ya Afya kwa Umma,Wizara ya Afya.
Rai imetolewa kwa wadau sekta ya Afya kuungana pamoja pindi wanapotekeleza miradi ya Afya ngazi ya jamii ili kuweza kutoa huduma bora na zenye ufanisi.
Rai hiyo imetolewa Wilayani Kibaha Mkoani Pwani na Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Pwani Bi.Savera Salvatory katika hafla ya majumuisho mara baada ya kutembelea mradi wa Afya Tek na Usimamizi Shirikishi juu ya Masuala ya Afya katika halmashauri na Manispaa ya Kibaha.
Bi.Savera amesema kuna wadau wengi wanaofanya kazi kwa kushirikiana na Serikali hivyo ni muhimu kuona namna ya kuwaunganisha pamoja huku akiupongeza mradi wa Afya –Tek kwa kuwa mwarobaini katika kutatua changamoto za afya katika jamii kwa halmashauri ya Kibaha na Manispaa ya Kibaha na kuongeza kuwa ni muhimu kuona namna ya kutoa motisha ili kuwezesha kufanya kazi kwa weledi huku akizungumzia umuhimu wa Bima ya Afya kwa Wote.
“Kuna wadau wengi wanaofanya masuala ya Afya tuone tunawajumuishaje hawa wadau ili kuweza ni namna gani ya kutoa motisha kwa wanaotoa huduma ngazi ya jamii na katika Bima ya Afya kwa Wote vichwani mwetu tuanze kutambua manufaa yake na tuendelee kuelimisha jamii “amesema.
Afisa Programu ,Elimu ya Afya kwa Umma,Wizara ya Afya Simon Nzilibili ametoa wito kwa wadau sekta ya Afya kuendelea kushirikiana katika uimarishaji wa utoaji huduma za Afya ngazi ya jamii.
“Wadau tukiendelea kushirikiana tutaendelea kuboresha huduma za afya ngazi ya jamii na hii itakuwa na matokeo chanya hasa katika uimarishaji wa mifumo”amesema.
Kiongozi wa Mradi wa Afya –Tek Dkt.Angel Dillip amesema mradi huo umeweza kufikia jamii kwa asilimia 91.
“Tumeweza kuwafikia watu laki mbili na elfu thelathini sawa na asilimia 91 katika maeneo haya mawili halmashuri ya Kibaha na Manispaa ya Kibaha na Afya Tek ipo sambamba kabisa kwa kushirikiana na serikali kuelekea Bima ya Afya kwa Wote kwani huduma ya afya -Tek inamfikia mpokea huduma (mgonjwa)moja kwa moja akiwa nyumbani kwa njia ya teknolojia ya kidijitali hawa watoa huduma ngazi ya jamii wamepewa hizo simu za kisasa katika utekelezaji wa majukumu yao”amesema.
Naye Mganga Mkuu Mkoa wa Pwani Dkt.Gunini Kamba amesema mradi wa Afya Tek umesaidia kupunguza vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga huku Afisa Ufuatiliaji na Tathmini Elimu ya Afya kwa Umma,Wizara ya Afya Erick Msunyaro akisema mradi huo umesaidia kupunguza gharama ya utumiaji wa karatasi
Ikumbukwe kuwa Mradi wa Afya-Tek unatekelezwa katika Halmashauri ya Kibaha na Manispaa ya Kibaha lengo likiwa ni kuchangia kupunguza vifo vya wajawazito,mama waliojifungua, na watoto chini ya miaka mitano na kuboresha afya za vijana balehe ambapo unatekelezwa kwa kushirikiana na Wizara ya Afya,TAMISEMI,Baraza la Famasi,Timu za Afya za Mkoa na Halmashauri na Mashirika yasiyo ya Kiserikali ya Apotheker na D-tree International .
Hivyo,mradi huu hutumia mfumo wa teknolojia ya kidijitali kuwaunganisha watoa huduma za afya katika ngazi ya jamii(WAJA),wahudumu wa maduka ya dawa muhimu(DLDM) na vituo vya huduma za afya na umeanza kutumika kuanzia Julai 2020 na hadi sasa umeunganisha watoa huduma ngazi ya Jamii 240,DLDM 149, vituo vya kutolea huduma za afya vya umma 39 na binafsi 10 .
Pia ,mradi huu ulitoa mafunzo kwa watumiaji wa mfumo takribani 500 ,vitendea kazi ikiwemo simu za mkononi 450 zenye mfumo wa Afya Tek.