Na WAF – Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi leo ameongoza Menejimenti na watumishi wa Wizara katika zoezi la upandaji miti katika Ofisi za Wizara (Jengo la Kitengo cha Elimu ya Afya) zinazoendelea kujengwa katika eneo la Njedengwa Jijini Dodoma.
Prof. Makubi amesema Wizara ya Afya pamoja na Taasisi zake inaendelea kuboresha mazingira kwa vitendo na kushiriki kikamilifu katika upandaji miti.
Hii ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha mazingira yetu hapa nchini kama ambavyo Makamu wa Rais Mhe. Phillip Isdor Mpango amekuwa akisisitiza kuwa Taasisi zote za Serikali ni vizuri ziwe mbele kuhamasisha wananchi kupanda miti, sisi hili agizo tumeanza kulitekeleza siku nyingi katika Taasisi zetu ikiwa pamoja na kwenye Hospitali” amesema Prof. Makubi.
Amesema zoezi hili la upandaji miti ni awamu ya tatu sasa na Wizata na Taasisi zake zitaendelea kuhakikisha mazingira yanalindwa kwa kupanda miti.
“Niendelee kutoa wito kwa Taasisi zetu ziendelee kupanda miti, nimeona Hospitali za Rufaa za Mikoa mbalimbali zinashiriki kwenye zoezi hili pamoja Tasisi zetu, kuna miti ya matunda, mbao pamoja na ya dawa yote haya tunayahitaji kwenye Sekta yetu” amesisitiza Prof. Makubi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Bi. Deodatha Makani amesema ni muhimu kwa watumishi kuunga mkono juhudi za Serikali kupanda miti ili kuboresha mazingira mahali pa kazi na kwenye makazi yao.
“Watumishi tunatumia muda mwingi tukiwa mahali pa kazi hivyo tuna kila sababu ya kuboresha mazingira, nawahamasiha watumishi na wananchi kwa ujumla kuendelea kuunga mkono upandaji miti ili kuweza kuboresha mazingira yetu” amesema Bi. Makani.
Jumla ya miti 100 imepandwa huku miti 400 ikitolewa kwa watumishi kwenda kupanda katika makazi yao.