Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya hali ya hewa nchini, (TMA), Dkt. Ladislaus Chang’a akizungumza na wadau wa mamlaka hiyo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili ili kuwaongzea uwezo katika Utabiri wa mvua za masimu. Kulia ni Mkurugenzi wa Huduma za utabiri Hamza Kabelwa na kushoto ni Dkt. Pascal Waniha Mkurugenzi wa Miundombinu na huduma za ufundi.
Wataalam wa Mamlaka ya hali ya hewa wakiwa katika majadiliano wakati wa mafunzo ya siku mbili ili kuwaongzea uwezo katika Utabiri wa mvua za masimu.
KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Ladislaus Chang’a amewataka watumishi wa TMA kutumia kauli mbiu ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa vitendo.
Dkt. Chang’a ameyasema hayo hivi karibuni, Kibaha Mkoani Pwani wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya kuwaongeza uwezo kwa wataalam wa TMA katika utabiri wa mvua za msimu.
“Watumishi wote mnatakiwa kuangalia namna gani tunaweza kuishi kwa vitendo kauli mbiu ya Kazi Iendelee kwa kuzingatia weledi na umahiri mkubwa, kauli ambayo Mhe. Rais amekuwa akiisisitiza kila wakati”. Amesema Dkt. Chang’a.
“Sisi, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) jukumu letu la msingi ni kutoa utabiri wa hali ya hewa hivyo mafunzo haya yatasaidia kuendeleza kazi yetu ya msingi na kutoka viwango tulivyopo kwenda viwango vya juu zaidi ikiwa ni maana halisi ya kazi iendelee”. Amesisitiza Dkt. Chang’a.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri, Dkt. Hamza Kabelwa amesema mafunzo hayo ni kwaajili ya kuwajengea uwezo wataalam wa TMA na kusaidia kuboresha huduma za hali ya hewa zinazotolewa kwa wadau mbalimbali.
Mafunzo hayo yamefadhiliwa na Taasisi ya Utafiti ya Norway ya Michelsen ambayo ni mtekelezaji wa mradi wa wa Huduma za Hali ya Hewa zinazozingatia jinsia kwa usalama wa chakula na lishe (COGENT) yakiwa na lengo la kuboresha huduma za hali ya hewa zinazotolewa na TMA kwa sekta mbalimbali katika kulinda maisha na mali za watu.