NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewataka Waandaji wa vyakula katika maeneo mbalimbali nchini pamoja na wananchi kwa ujumla kuhakikisha usalama wa chakula wanachokiandaa ili kuweza kumlinda mlaji au walaji wa chakula hicho.
Akizungumza leo Februari 10,2023 Jijini Dar es Salaam, Kaimu Meneja Kitengo cha Tathmini ya Vihatarishi vya Chakula Dkt. Ashura Kilewela amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuzingatia usalama wa chakula kwani usalama wa chakula ni jukumu la kila mmoja wetu .
Dkt.Ashura ameongelea juu ya kutenganisha chakula kibichi na chakula kilichoiva ili vimelea katika chakula kibichi visiweze kuingia katika chakula kilichoiva na kuweza kumletea madhara mlaji au walaji wa chakula hicho.
Amesema katika kuhakikisha chakula kinakuwa salama kuna ulazima wa kutumia maji na malighafi salama kwani katika uandaaji wa chakula usipotumia malighafi salama uwezekano wa kuhamisha ule uchafuzi ni mkubwa.
“Mfano umeandaa nyama ambayo imetokana na mfugo ambao umetumia madawa yasiyo salama au kuna mabaki ya dawa za mifugo katika nyama ile hauna namna wewe muandaaji wa chakula kutoa yale mabaki ya dawa katika chakula kwahiyo ni msingi muhimu kuzingatia utumiaji wa malighafi iliyosalama”. Amesema Dkt.Kilewela.
Pamoja na hayo amesema wanashirikiana na Wizara pamoja na Taasisi mbalimbali kutoa elimu na kuhakikisha wakulima mashambani wanaelewa athari za matumizi ya dawa kwenye chakula na kuhakikisha chakula wanachokizalisha ni salama .