Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Huduma za Meli Nchini (MSCL) Eric Hamissi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya kushushwa majini Meli ya Mv Mwanza hapa kazi tu Feburuari 12 mwaka huu
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Huduma za Meli Nchini (MSCL) Eric Hamissi akizungumzia hafla ya kushushwa majini Meli ya Mv Mwanza hapa kazi tu
Muonekano wa Meli ya Mv Mwanza hapa kazi tu itakayoshushwa majini Feburuari 12 mwaka huu kwaajili ya kuendelea na hatua nyingine za ujenzi
****************************
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Meli ya Mv Mwanza hapa kazi tu inayoendelea kujengwa katika Bandari ya Mwanza Kusini inatarajiwa kushushwa majini Feburuari 12 mwaka huu.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Huduma za Meli nchini (MSCL) Eric Hamissi, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Alhamisi Feburuari 9,2023 ikiwa zimesalia siku chache Meli hiyo kushushwa majini.
Hamissi ameeleza kuwa kuna hatua tatu za ujenzi wa Meli ambapo hatua ya kwanza ni kuweka Msingi (KEEL LAYING) ya pili ni ya kushusha kwenye maji na ya tatu ni kujaribu mitambo ya ndani na kuanza safari ya majaribio kabla ya kuanza safari rasmi.
Amesema ujenzi ma Meli hiyo umefikia asilimia 82 na kazi iliyobakia ni kuweka vyoo, kupaka rangi, kuweka vitanda, kufunga viyoyozi,kuweka singibodi pamoja na kufunga mitambo ya kuendeshea Meli kwa Kepteni.
“Wakati Serikali ya awamu ya sita inaingia madarakani Meli hii ilikuwa asilimia 42 kipindi cha miezi 22 ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassani fedha nyingi zilitolewa hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 82 hivyo naipongeza sana Serikali kwa namna inavyojitahidi kutekeleza miradi ya kimkakati”, amesema Hamissi
Aidha, ameeleza kuwa kushushwa kwa Meli hiyo haimaanishi kuwa huduma zitaanza kutolewa kwa sasa bali ni hatua ya kuhakiki ubora wa umbo la Meli kama linavujisha maji huku akisema wanatarajia kukabidhiwa Meli hiyo Agosti mwaka huu.
Hamissi ameeleza Meli itakuwa na uwezo wa kusafiri kwenye Bandari zote kubwa ikiwemo Jinja,Uganda, Kisumu,Kemondo, Bukoba na endapo soko litaruhusu watafika hadi Musoma na itakuwa na uwezo wa kusafiri kwa haraka kutokana na injini zake kuwa kubwa.
“Meli ya Mv Mwanza hapa kazi tu itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1200,Tani 400 za mizigo pamoja na magari 20 yakiwemo makubwa matatu”,amesema Hamissi
Mwisho alieleza kuwa kukamilika kwa Meli hiyo kutasaidia kurahisisha shughuli za usafirishaji wa watu,mizigo nchini na nje ya nchi sanjari na kuchochea ajira.