Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu maswali, Bungeni jijini Dodoma, Februari 9, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………………..
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan iko makini na itaendelea kufuatilia miradi yote inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini ili kudhibiti matumizi mabaya ya mali ya umma.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali kupitia ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ya mipango na shughuli za Serikali na sasa watendaji wake wanapita katika mamlaka za Serikali ili kufanya tathimini, kujiridhisha kuhusu thamani ya fedha katika miradi inayotekelezwa.
Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Februari 9, 2023) wakati akijibu swali la Mbunge wa Arumeru Magharibi Noah Saputu, katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu Bungeni Jijini Dodoma. Mbunge huyo alitaka kujua kauli ya Serikali kuhusu wizi na ubadhirifu katika miradi ya umma.
Waziri Mkuu amesema Serikali ina mfumo wa kufanyia tathmini na mapitio ya mwenendo wa matumizi ya mali na fedha za umma pamoja na kufanyia kazi mapendekezo ya taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inayotolewa baada ya kufanya ukaguzi na kubaini mapungufu kwenye baadhi ya miradi.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali imekuwa ikitoa misamaha au ruzuku pale inapojiridhisha kuwa panahitajika kufanya hivyo, mfano hivi karibuni baada ya mbolea kupanda bei ilitoa ruzuku ya shilingi bilioni 150 kwenye mbolea ili kuhakikisha bidhaa hiyo inapatikana kwa wakulima kwa gharama nafuu.
Amesema Serikali itaendelea kuhakikisha maeneo yote yanayopata misamaha au ruzuku yanaratibiwa na kusimamiwa kwa ukaribu ili kudhibiti mfumuko wa bei. Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Zaituni Swai aliyetaka kujua mikakati ya Serikali katika udhibiti wa bei ya soko pale misamaha inapotolewa.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema suala la ucheleweshwaji wa fidia kwa wananchi ambao maeneo yao yamechukuliwa kwa ajili ya kupisha miradi mbalimbali ya maendeleo linatokana na taratibu zinazotakiwa kufuatwa kabla ya ulipaji wa fidia ikiwemo kujiridhisha ni nani mmiliki sahihi wa eneo husika.
Waziri Mkuu amesema wananchi wote waliochukuliwa maeneo yao kupisha ujenzi wa miradi ya maeneleo watalipwa stahiki zao. Ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Kigoma Mjini, Kirumbe Ng’enda aliyetaka kujua msimamo wa Serikali kuhusu ucheleweshaji wa ulipaji wa fidia kwa wananchi wanaochukuliwa maendeo yao.