Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imeshauriwa kutoa elimu ya kutosha kwa vijana nchini ili kunufaika na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
Pamoja na ushauri huo, imepongezwa kwa kuandaa mwongozo wa mfuko huo Mwaka 2022 ili kuruhusu kijana mmoja mmoja kukopa badala ya vikundi peke yake.
Hayo yamesemwa leo na Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Dkt.Joseph Mhagama alipokuwa akiwasilisha taarifa ya mwaka ya shughuli za kamati kwa kipindi cha kuanzia Februari 2022 hadi Januari, 2023.
“Moja ya malengo ya mfuko huo ni kuwawezesha vijana nchini wenye umri kati ya Miaka 15 hadi 35 kupata mitaji kwa njia ya mikopo yenye masharti nafuu ili kuanzisha au kuendeleza miradi yao ya uzalishaji mali.”
Pia kuna umuhimu wa kutathmini vigezo vilivyowekwa ili vijana wengi zaidi wanufaike na mradi na kuongeza thamani ya Mfuko kwa kuuongezea fedha.
“Kamati inaipongeza Serikali kwa kuendelea kusikiliza maoni ya Wabunge kuhusu namna bora za kuweka mifumo ya kitaasisi ambayo itachangia juhudi za kuwasaidia vijana wa nchi hii kujikwamua kiuchumi kwa mustakabali mpana wa maendeleo ya nchi yetu.”