Naibu waziri wa nchi ofisi ya Rais utumishi wa umma ,Deogratius Ndejembi akizungumza katika kikao kazi cha 3 cha serikali mtandao kinachofanyika jijini Arusha.
Washiriki wa kikao hicho kilichoandaliwa na Mamlaka ya serikali mtandao kutoka mikoa mbalimbali kinachoendelea jijini Arusha.
Katibu Mkuu ofisi ya Rais utumishi ,Laurian Ndumbaro akizungumza katika kikao hicho jijini Arusha leo.
**********************
Julieth Laizer,Arusha.
Arusha.Naibu waziri wa nchi ofisi ya Rais utumishi wa umma ,Deogratius Ndejembi amezitaka taasisi zote za umma nchini kuendana na kasi ya mabadiliko kwa kufanya shughuli zake kwa kutumia mfumo wa Tehama.
Ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati akifungua kikao kazi cha 3 cha serikali mtandao kilichoandaliwa na Mamlaka ya serikali mtandao (eGA) kilichowashirikisha watumishi wa umma kutoka mikoa mbalimbali ,huku kauli mbiu ikiwa ni “Mifumo jumuishi ya TEHAMA kwa utoaji bora wa huduma za umma.”
Amesema kuwa,utoaji wa huduma kwa taasisi za umma kutumia mfumo wa Tehama bado zipo chini hivyo ni wakati sasa wa kuhakikisha taasisi hizo zinatumia mfumo huo kuwafikishia wananchi wake huduma ili kuendana na kasi ya mabadiliko.
Ndejembi amewataka wakuu wote wa taasisi za umma kuhakikisha wanajiunga na mfumo huo ili kuendana na kasi ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutaka huduma zote zifikie wananchi kupitia mfumo wa kidigitali.
“Niwaombe pia mhakikishe mnapeleka huduma karibu na wananchi kupitia mfumo wa Tehama ili kuwarahishia wananchi kupata huduma hizo kwa haraka na kwa wakati “amesema Ndejembi.
Amefafanua kuwa, endapo taasisi nyingi zitautumia mfumo huo zitasaidia sana kuondoa urasimu kwa kutumia makaratasi kwani shughuli nyingi duniani hivi sasa zinatolewa kwa kutumia Tehama na zimefanikiwa kwa kiwango kikubwa sana.
Aidha alitoa wito pia kwa taasisi binafsi nazo kujitahidi kutumia mfumo huo wa serikali mtandao kwani una manufaa makubwa katika utoaji wa huduma kwa wananchi .
Katibu Mkuu ofisi ya Rais utumishi ,Laurian Ndumbaro amewataka wakuu wa taasisi kujitahidi kubadili website zao ili ziendane kisasa ,huku akitaka vikao mbalimbali vya bodi vinavyofanyika kuhakikisha vinafanyika kidigitali.
“Ifike wakati sasa hata baraza la madiwani ,vikao mbalimbali vya halmashauri na katika majiji zifanyike kidigitali ili serikali yetu iwe serikali ya mtandao na tuhakikishe tunashuka hadi huko chini kwa wananchi wote .”amesema Ndumbaro.
Naye Mkurugenzi wa Mamlaka ya serikali mtandao (eGA) ,Mhandisi Benedict Ndomba amesema kuwa,wamekuwa wakifanya kazi zao kwa weledi ,ubunifu,na ushirikiano pamoja na kufanya kazi kwa pamoja katika kutoa elimu kuhusu serikali mtandao.
Amesema kuwa,wamekuwa wakifanya ukaguzi wa mifumo na miundombinu ya Tehama ambapo mamlaka hiyo imeweza kusimamia kikamilifu miundombinu ya mtandaoni.
Aidha ametaja changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni pamoja na upungufu wa wataalamu wa Tehama ambapo wadau wa serikali mtandao kupitia kikao hicho kwa pamoja wataweza kuweka mikakati namna ya kukabiliana na changamoto hizo.