MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi na Bahari Kuu Dkt.Emmanuel Andrew Sweke,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Februari 8,2023 jijini Dodoma wakati akielezea utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo.
WAANDISHI wa habari pamoja na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari – MAELEZO, Bi. Zamaradi Kawawa wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi na Bahari Kuu Dkt.Emmanuel Andrew Sweke, wakati akielezea utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo leo Februari 8,2023 jijini Dodoma.
MKURUGENZI Msaidizi wa Idara ya Habari – MAELEZO, Bi. Zamaradi Kawawa,akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi na Bahari Kuu Dkt.Emmanuel Andrew Sweke, kutoa maelezo juu ya utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo leo Februari 8,2023 jijini Dodoma.
……………………….
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi na Bahari Kuu Dkt.Emmanuel Andrew Sweke,ameeleza kuwa katika kipindi cha mwezi Julai 2022, hadi Februari mwaka huu Mamlaka hiyo imekusanya Sh.bilioni 4.1 ikiwa ni mapato yatokanayo na utoaji wa leseni kwa ajili ya meli za uvuvi na huduma nyingine.
Hayo ameyasema leo Februari 8,2023 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shuguli mbalimbali za Mamlaka hiyo.
Dk. Sweke, amesema Mamlaka hiyo ina jukumu la kutoa leseni kwa ajili ya uvuvi wa bahari kuu kwa meli za ndani na nje pamoja na kulinda,kusimamia na kuratibu shughuli zote za uvuvi wa bahari kuu.
Amesema kuwa makusanyo hayo yamevunja rekodi iliyowekwa na Mamlaka hiyo kwa kipindi cha miaka saba iliyopita.
“Makusanyo makubwa ya mwisho yalikuwa ni Sh. bilioni 4 katika kipindi cha mwaka 2015/2016 lakini yalishuka sana baada ya kuletwa kwa kanuni ambayo ilikuwa inawataka wavuvi kutoa muraba wa dora 0.4 kwa kila kilo moja ya samaki.
“Hali hii ilisababisha makusanyo kushuka sana kutokana na meli nyingi za uvuvi kukimbia na kuacha kufanya uvuvi katika nchi yetu lakini kutokana na hali hiyo tulijifungia na kuondoa kanuni hiyo na sasa matunda yanaonekana kwa kupanda kiasi cha ukusanyaji wa mapato yatokano na utoaji wa leseni za uvuvi na huduma nyingine zinazotolewa na mamlaka hii”amesema Dk. Sweke
Aidha, amesema kuwa katika kulinda usalama wa bahari kuu wameweka mifumo ya kulinda usalama ikiwa ni pamoja na kutumia mifumo ya kufuatilia meli ndani ya maji na kutumia doria za ndege kwa ajili ya kuangalia kinachofanyika.
“Mifumo hii tunayotumia sasa pamoja na kufanya doria kwa kutumia ndege zimesaidia sana kukomesha vitendo vya uvuvi harafu bahari kuu”amesema Dk. Sweke
Hata hivyo amesema toka Mamlaka kuanzishwa imefanikiwa kukamata meli moja iliyokuwa na samaki tani 100 ya samaki wasiolengwa.