KONGAMANO la mjadala wa uvumbuzi unatarajia kuanza Februari 9,2023 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambapo mambo mbalimbali yataangaziwa ikiwemo Tafiti na Ubunifu ili kuweza kutatua changamoto zilizopo katika jamii.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo Februari 8,2023 jijini Dar es Salaam ,Mkurugenzi wa Ofisi ya Makamu wa UDSM,Dkt Salvatory Nyanto amesema chuo hicho kimepata heshima ya kuandaa mjadala ambao umekuwa sehemu ya majukumu makuu ya ufundishaji ujifunzaji,utafiti, ubunifu na utoaji huduma kwa jamii.
“Tunaangali ni namna gani tunaweza kuwafikia jamii na kutatua changamoto kupitia tafiti,majadiliano na mafunzo na hili ni lengo la Chuo hiki kikongwe ambacho mwaka jana kiliadhimisha miaka 60 ya ufundishaji,ujifunzaji,utafiti na ubunifu lakini pia utoaji huduma kwa jamii,” amesema
Dkt. Nyanto alisema kwa Upande wa Taasisi ya Kimataifa ya Japan (JICA) pia imetimiza miaka 60 ya utoaji huduma nchini na hilo linadhihirisha mahusiano ya muda mrefu na imekuwa mstari wa mbele kusaidia maendeleo na kuhudumia wananchi.
“Mjadala wa siku mbili ni fursa kwa UDSM na Watanzania kujifunza sio tu mahusiano ya Japana na Tanzania pia unatoa fursa kujifunza kujadili masuala ,uvumbuzi na ujasiriamali na kuendeleza ajenda ya nchi ambayo siku zote ni kufikia watanzani na kuwahudumia,”ameeleza.
Alibainisha kuwa Mjadala huo pia unaakisi dira ya UDSM ya mwaka 2061 ambayo inajikita katika kuongeza mashirikiano ya kitaalumu na kuongeza wigo wa umataifishaji,ufundishaji,ujifunzaji pamoja na uvumbuzi.
“Tunawashukuru na tunawakaribisha Watanzania kuja kujifunza masuala yatakayojadiliwa katika kongamano hilo,”alisisitiza Dk Nyanto.
Kwa Upande wake Mwakilishi wa JICA,Yamamura Naofuma alisema kongamano hilo litaanza Februari 9 hadi 10 na itawaleta pamoja wanataalamu wa Tanzania na Japani kubadilishana uelewa na uzoefu katika masuala ya Uvumbuzi kupitia majadiliano.
Alisema kauli mbiu ya Kongamano hilo no ‘Uvumbuzi kwa Uchumi wa nchi na Maendeleo Endelevu’ ambapo mgeni rasmi katika Kongamano hilo anatarajiwa kuwa Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia.
“Tukio hili litatoa nafasi kubwa kupata ufafanuzi wa changamoto kupitia uvumbuzi ambao utasaidia ukuaji wa taifa na Maendeleo endelevu litakuja na suluhu kwa kesho nzuri kwa Taifa kwa ujumla.
Pia alieleza kuwa itakuwa fursa ya kupata picha halisi ya changamoto,fursa na njia sahihi ya jinsi ya Tanzania inaweza kutumia uvumbuzi kwa Maendeleo na Japan imeweza vipi kufanikisha uvumbuzi katika sekta ya kilimo.
“Washiriki watapata nafasi ya kusikia na kujifunza siri za mafanikio ya Japan kupitia wataalamu wake ,wataalamu waliobobea katika masuala ya uvumbuzi na baadhi ya wajumbe wa JICA alumni,”alieleza Naofum.