Baadhi ya wanafunzi hasa wa shule za Sekondari wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro wanalazimika kutumia muda mwingi kwenye shughuli za utafutaji kwa kuelemewa na majukumu ya kutunza familia (Walezi wao) miongoni mwa sababu zinazochangia kudhorota kwa elimu kwakua hakuna ufuatiliaji wa karibu wa wazazi.
Kwa nyakati tofauti baadhi ya walimu walipokuwa kwenye vikao na Mkuu wa Walaya ya Same Kasilda Mgeni, wakati wa ziara yake kufuatilia mwenendo wa kuripoti kwenye shule walizopangiwa wanafunzi wa kidato cha kwanza, Walisema asilimia kubwa ya wazazi na walezi ni kama wamewatekeleza watoto wao kwani hakuna ufuatiliaji.
“Unakuta mtoto haonekani shule karibia wiki nzima, sisi tunachokifanya siku akija tunamwambia amlete mzazi mzazi haonekani, ukimdadisi sana ndio unakugundua anaishi na Bibi ambae ni mzee sana hata kutembea hawezi , na wazazi wake wanaishi maeneo mengine muda mwingi mtoto anakua ndie mtafutaji”.Alisema Minja Elius Mkuu wa shule ya Sekondari Kwakoko.
Walimu hao walisema pamoja na kuwa asilimia kubwa ya wanafunzi kidato cha kwanza wamekwisha ripoti baadhi yao ambao bado hawajulikani walipo ni wale ambao wamekosa ushiriki wa Moja kwa moja wa wazazi kwakua huishi na walezi hasa Bibi zao ambao wenyewe pia hawajiwezi.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Same Kasilda Mgeni ameagiza wakuu wa shule kuwasilisha majina ya wanafunzi ambao bado hawajaripoti kwa ajili ya taratibu nyingine za kisheria.
“Kwenye hili la wanafunzi ambao bado hawajaripoti, sikumbili zinawatosha wakuu wa shule nipate majina ya wanafunzi wote tuanze ufuatiliaji lazima tujue walipo”.Alisema Kasilda Mgeni Mkuu wa Wilaya ya Same.
“Binafsi sitaki kabisa kuona tukitajwa vibaya kwenye Elimu, Same inachukua asilimia 40 ya eneo lote la mkoa wa Kilmanjaro kwa ukubwa huo huo lazima tufanye pia Makubwa kwenye Elimu wakati nahangaika kutafutia suluhu changamoto mlizonazo walimu pia mtimize wajibu wenu”.Alisema Kasilda.
Kwa mujibu wa taarifa ya Afisa elimu Sekondari wa halmashauri hiyo ya Wilaya ya Same zaidi ya asilimia 90 ya wanafunzi wa kidato cha kwanza wamekwisha Ripoti mpango wa sasa ni kufuatilia ambao bado hawajaonekana ingawa taarifa za awali zinaonesha wengi wao wamehamishiwa shule nyingine.