**************************
Na. WAF – DAR – ES SALAAM
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema Kituo cha Huduma za Upandikizaji Mimba Kairuki Green IVF, Bunju kitatatua changamoto ya Watanzania kwenda nje ya nchi kwa gharama kubwa kufata huduma hizo.
Dkt. Mwinyi amebainisha hayo leo Jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa Kituo cha Huduma za Upandikizaji Mimba Kairuki Green IVF, kilichopo Bunju jijini Dar Es Salaam.
Amesema katika kukabiliana na changamoto hiyo baadhi ya Watanzania wamekuwa wakilazimika kutafuta huduma za upandikiza mimba nje ya nchi na kwa gharama kubwa.
Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa nidhahiri wananchi wachache tu wenye uwezo ndio wanaomudu lakini walio wengi wanashindwa kupata huduma hizo.
Aidha amesema hakika tukio hilo ni muhimu, ushahidi wa dhamira na jitihada za taasisi hii za kuunga mkono jitihada za Serikali za kuimarisha huduma za afya zinazotolewa hapa Tanzania jambo ambalo lilikuwa harakati za Hayati Dkt Kairuki enzi za uhai wake.
Dkt. Mwinyi ameendelea kusema afya ya uzazi ni jambo ambalo Hayati Prof. Kairuki aliliwekea uzito mkubwa, huenda alifanya hivyo kutokana na changamoto inayowakabili kina mama wengi kutopata ujauzito.
“Nitoe shukrani za dhati kwako Mwenyekiti wa Taasisi ya Afya na Elimu mama Kairuki kwa kunialika kuja kujumuika nanyi katika tukio hili la ufunguzi wa kituo hiki cha Kairuki Green IVF na kumbukumbu ya mzee wetu Hayati Prof. Kairuki.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa Serikali ipo tayari kushirikiana na Sekta binafsi katika kuhakikisha wanatatua tatizo la ugumba nchini ili wananchi wapate huduma bora za matibabu hayo.
Waziri Ummy amesema ukubwa wa Tltatizo la ugumba nchini Tanzania linaanzia asilimia 30 na linafika mpaka asilimia 80.
“Natambua ukubwa wa tatizo hili na sisi wenyewe kama Serikali hatuna hata kituo kimoja cha kutoa huduma hizo”, ameeleza Mhe. Ummy
Mhe. Ummy amesema Wizara ya Afya tutaendelea kushirikiana na Kairuki Green IVF kuhakikisha kwamba wanawafikia Watanzania wengi ili kutoa huduma bora za matibabu na linapokuja swala la Afya ni kipaumbele chao.
Waziri Ummy amempongeza Dkt. Mwinyi kwa utendaji mzuri katika mapinduzi makubwa yanayofanyika kule Zanzibar katika upande wa afya kwa kweli wanajivunia mafanikio hayo.
Vile vile amesema watahakikisha Serikali ya awamu ya sita, ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa Sekta binafsi kuweza kutoa huduma za afya hususani afya ya mama na mtoto.