Mkuu wa wilaya ya Mbinga Aziza Mangosongo akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya ukarabati na matengenezo ya barabara kwa kutumia Teknolojia stahiki ya nguvu kazi kwa vikundi vya wanawake na vijana yaliyoendeshwa na chuo cha Ukandarasi ATTT-Mbeya
Baadhi ya vijana waliohitimu mafunzo ya ukandarasi wilayani Mbinga wakimsikiliza Mkuu wa wilaya hiyo Aziza Mangosongo(hayupo pichani).
Mwenyekiti wa wahitimu wa mafunzo ya ukarabati na matengenezo ya barabara kwa kutumia Teknolojia stahiki ya nguvu kazi Betram Kapinga akisoma risala ya wahitimu hao.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga Aziza Mangosongo kushoto akimpa cheti mhitimu wa mafunzo hayo Eustella Manga.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Ovans Contruction LTD Valence Urio akitoa nasaha kwa wahitimu wa mafunzo hayo ambapo amewataka kwenda kuwa waadilifu,waaminifu na kutanguliza maslahi ya Taifa mbele katika kazi zao.
Mkuu wa wilaya ya Mbinga Azazi Mangosongo kushoto,akitoa cheti cha pongezi kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Ovans Contruction Ltd Valence Urio kutokana na mchango wake uliofanikisha kufanyika kwa mafunzo ya ukarabati na matengenezo ya barabara kwa kutumia Teknolojia stahiki ya nguvu kazi kwa vikundi vya wanawake na vijana wilayani humo.
Mkufunzi wa mafunzo ya ukarabati na matengenezo ya barabara kwa kutumia teknolojia stahiki ya nguvu kazi kutoka Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi ICOT-Mbeya Donatha Kamwella akitoa taarifa ya mafunzo hayo.
……………………………..
Na Muhidin Amri,Mbinga
MKUU wa wilaya ya Mbinga Aziza Mangosongo,amezitaka taasisi zinazosimamia sekta ya ujenzi wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) na Tarura,kutowapa kazi wakandarasi wabovu na wenye Historia mbaya ya kujenga na kukarabati barabara chini ya viwango.
Amesema,wakandarasi hao wanasababisha hasara kubwa kwa serikali kwa kuwa inalazimika kufanya matengenezo ya barabara mara kwa mara na kutumia fedha nyingi ambazo zingepelekwa kujenga miradi na kuboresha huduma nyingine za kijamii.
Badala yake Mangosongo,ameitaka TANROADS na Tarura, kuwapa kazi wakandarasi walioonyesha uwezo mkubwa katika ujenzi wa miradi ya barabara wakiwemo makundi ya vijana na wanawake waliopata mafunzo ya kujenga miradi ya barabara.
Mangosongo ametoa kauli jana,wakati akifunga mafunzo ya mwezi mmoja ya ukarabati na matengenezo ya barabara kwa kutumia teknolojia stahiki ya nguvu kazi kwa vikundi vya wanawake na vijana wilayani Mbinga yaliyotolewa na taasisi ya teknolojia ya ujenzi ICOT-Mbeya.
Amesema,vijana hao kama watatumika vizuri watakuwa msaada mkubwa kwa serikali katika ujenzi wa miundombinu ya barabara za wilaya na mkoa wa Ruvuma kwa gharama nafuu,badala ya kuwatumia wakandarasi wababaishaji,wasiokuwa na uwezo na uzalendo kwa nchi yao.
Aidha Mkuu huyo wa wilaya,amewaasa vijana hao kwenda kufanya kazi kwa bidii na nidhamu ili waweze kupewa miradi mingi na hivyo kukuza fani ya ukandarasi katika sekta ya ujenzi wa barabara na hata majengo.
“nawahakikishia serikali ya wilaya,itakuwa bega kwa bega na nyinyi ili mafunzo haya mliyoyapa yakatumike kikamilifu katika miradi ya ujenzi wa barabara katika wilaya yetu ya Mbinga na mkoa wa Ruvuma na kuwakomboa kiuchumi”alisema Mangosongo.
Katika hatua nyingine Mangosongo ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani humo,ameziagiza Halmashauri za wilaya ya Mbinga na Halmashauri ya Mji Mbinga kuwapa mikopo vijana hao kama njia ya kuwajengea uwezo ili waweze kutumia elimu waliopata kukuza uchumi binafsi wilaya na Taifa.
Ametoa ushauri kwa Halmashauri hizo,kuwa na utaratibu wa kuwapa elimu ya ujasiriamali kwanza kabla ya kutoa mikopo kwa vikundi ili fedha zinazotolewa ziweze kufanya kazi iliyokusudiwa ya kuwaondolea wananchi waliojiunga kwenye vikundi na umaskini,badala ya kutumika kinyume na malengo ya serikali.
Kwa upande wao washiriki waliohitimu mafunzo hayo kupitia risala iliyosomwa na Betram Kapinga,wameiomba serikali kuwapa fursa zaidi katika kazi za ujenzi wa barabara ili kuwajengea uwezo na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi binafsi na Taifa.
Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Ovans Contruction Ltd Valence Urio, amewataka wahitimu hao kuwa waadilifu,waaminifu,kuwa na uthubutu na kutanguliza maslahi ya Taifa wanapotekeleza miradi ya ujenzi wa barabara badala ya kutanguliza maslahi binfasi.
Jumla ya vijana 17 kati yao wanaume 11 na wanawake 6 wameshiriki katika mafunzo hayo, yenye lengo la kuwawezesha vijana wakandarasi waliojiunga kwenye vikundi kushiriki katika ujenzi wa barabara kwa kutumia teknolojia stahiki ya nguvu kazi.