Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) akijibu swali bungeni jijini Dodoma.
……………………………………..
Na Farida Ramadhani, WFM – Dodoma
Serikali imetoa rai kwa wanahisa wa kampuni mbalimbali nchini kushiriki vikao vya mwaka vya wanahisa vya kampuni zao ili kuwa sehemu ya maamuzi yanayotolewa kwenye Mkutano Mkuu wa Mwaka.
Rai hiyo limetolewa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande alipokuwa akijibu swali la Mbunge Viti Maalum (CCM), Mhe. Ng’wasi Damas Kamani alitaka kujua kauli ya Serikali kwa kampuni binafsi zinazouza hisa kupitia soko la hisa na hazijatoa gawio kwa miaka mingi pamoja na kujiendesha vizuri.
Mhe. Chande alisema ulipaji wa gawio kwa wanahisa wa kampuni unafanyika kwa kuzingatia Kifungu cha 180 cha Sheria ya Kampuni, Sura 212.
Alibainisha kuwa kwa mujibu wa Sheria hii, Serikali haiwezi kuingilia maamuzi na taratibu za Kampuni kulipa gawio.