******************************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MAADHIMISHO ya kusherehekea wiki ya miaka 46 ya kuzaliwa katika Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, yamefana kupitia wanachama wake kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo.
Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika Kitongoji cha Kidomngen Kata ya Naberera, mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro Kiria Ormemei Laizer, yalihudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Simanjairo Dkt Suleiman Hassan Serera.
Katibu wa CCM Wilaya ya Simanjiro Amos Shimba amesema maadhimisho hayo yamehusisha matukio mbalimbali ikiwemo upandaji wa miti, ukaguzi wa nyumba ya mwalimu kwenye shule shikizi ya msingi Kidomngen, kugawa kadi za kielekroniki na kuhitimishwa kwa pambano la soka baina ya Naberera SC na shule ya sekondari Naberera.
Akizungumza kwenye maadhimisho hayo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro Kiria Ormemei Laizer amesema miaka 46 ya kuzaliwa CCM inaakisi ipasavyo maendeleo ya wananchi katika sekta mbalimbali.
“Rais Samia Suluhu Hassan amefanikisha maisha bora kwa kila Mtanzania kupitia shule, zahanati, vituo vya afya, maji na miundombinu mbalimbali,” amesema Kiria.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Dkt Suleiman Hassan Serera amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini na kumpa dhamana ya kuendelea kuongoza Wilaya hiyo.
Dkt Serera amewashukuru pia viongozi na wananchi wa Simanjiro kwa namna wanavyompa ushirikiano katika kutimiza majukumu yake.
Mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa kupitia Wilaya ya Simanjiro, Lenganasa Soipey amesema shina la kitongoji cha Kidomngen linatakiwa liwe Tawi.
Diwani wa Kata ya Naberera Marco Munga ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo madarasa ya shule.
Diwani wa Kata ya Ngorika Albert Msole amesema hivi sasa Wilaya hiyo imepata Mwenyekiti makini ambaye ameweza kufanya ziara katika Kata mbalimbali na kuwashukuru wanachama kwa kuchaguliwa kushika nafasi hiyo.
Diwani wa Kata ya Endiamtu, Lucas Chimba Zacharia amesema Simanjiro mpya ya maendeleo inaonekana kupitia chama hicho madhubuti.
Diwani wa Kata ya Mirerani Salome Nelson Mnyawi amempongeza Mwenyekiti Kiria kwa kusimama imara katika uongozi wake tangu achaguliwe.
Diwani wa Kata ya Naisinyai Taiko Kurian Laizer ameeleza kuwa uongozi wa awamu ya sita unaoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan umeonyesha kwa vitendo maendeleo ya wananchi.
Diwani wa kata ya Loiborsoit Siria Baraka Kiduya amesema Mwenyekiti Kiria anaongoza chama hicho ipasavyo kwenye wilaya hiyo kwani anajitahidi kuondoa makundi.