Taarifa za fedha za robo ya mwisho ya mwaka 2022 zinadhihirisha mafanikio makubwa yaliyopatikana kwa mwaka 2022 ambao ulikua mwaka wa mwisho wa utekelezaji wa mkakati wake wa Benki wa miaka mitano wa mwaka 2018 hadi 2022.
Kutokana na faida nzuri iliyopatikana ndani ya kipindi hicho ambayo imeongezeka kwa takriban mara 10, gawio kwa wanahisa nalo limepanda.
Taarifa za fedha za CRDB, zinaonesha mwaka 2022 ambao ulikua mwaka wa mwisho wa utekelezaji wa mpango mkakati wa biashara, kulikuwa na ufanisi katika maeneo karibu yote.
Faida baada ya kodi iliongezeka kwa asilimia 31 na kufika Sh353 bilioni mwaka 2022 kutokana na juhudi makini zilizoelekezwa katika ukuza mapato yasiyo yasiyotokana na mtaji.
“Mizania yetu imeendelea kuwa imara na kutuweka nafasi ya kwanza sokoni kutokana na kuongezeka kwa mikopo tuliyoitoa kwa wateja wetu na tunaamini kuendelea kuimarika kwa biashara baada ya wimbi la UVIKO-19 kutaendelea kutupa matokeo mazuri kama taasisi na nchi kwa ujumla,” alisema Nsekela.
Faida miaka mitano
Ongezeko hilo la faida lilitokana na ufanisi uliojionyesha maeneo kadhaa uliochangiwa na usimamizi makini wa uendeshaji.
“Tumepunguza uwiano wa gharama za uendeshaji na mapato yetu kutoka asilimia 67.4 mwaka 2017 mpaka asilimia 49.4. Hata kiwango cha mikopo chechefu nacho tumekipunguza kwa kiasi kikubwa,” alisema Nsekela.
Uwiano wa mikopo chechefu wa benki hiyo umepungua kutoka asilimia 12.4 mwaka 2017 mpaka asilimia 2.8 hivyo kuwa ndani ya masharti ya kikanuni yanayotaka usizidi asilimia tano.
Uwiano wa mikopo chechefu umepungua licha ya kiwango cha mikopo iliyotolewa kuongezeka kwa asilimia 138 kutoka Sh2.89 trilioni ya mwaka 2017 mpaka Sh6.87 trilioni mwaka 2022 hivyo kupandisha faida ya mtaji kutoka asilimia 4.8 mpaka asilimia 26.1 katika kipindi hicho.
Kutokana na ufanisi huo, bei ya hisa za CRDB imeimarika katika Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) ikipanda kutoka Sh160 mpaka Sh395 sawa na asilimia 147.
Mwenendo huo umewashawishi wanahisa kuendelea kuwekeza zaidi katika taasisi hiyo kubwa ya fedha nchini hivyo kupandisha mtaji wao kwa asilimia 102 kutoka Sh733 bilioni mpaka Sh1.47 trilioni katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Imani hiyo haiendi bure kwani gawio lao linatarajiwa kuongezeka zaidi mwaka huu pindi watakapoidhinisha kugawana asilimia 35 ya faida iliyopatikana baada ya kodi kwenye mkutano mkuu utakaofanyika Mei mwaka huu.
Ilipopata faida ya Sh36 bilioni mwaka 2017, benki hiyo ilitenga gawio la Sh5 kwa kila hisa ambalo lilipanda mpaka Sh36 kutokana na faida ya Sh268 bilioni iliyoipata mwaka 2021. Faida hiyo mwaka 2022 imefika Sh351 bilioni hivyo kutoa hakikisho la gawio nono zaidi.
Akizungumzia ufanisi wao uliopandisha thamani ya mali za benki kwa asilimia 97 kutoka Sh5.9 trilioni mwaka 2017 mpaka Sh11.64 trilioni mwaka 2022, Mkurugenzi wa Uhusiano wa Umma wa CRDB, Tully Mwambapa alisema wakati Nsekela anajiunga nao alileta falsafa ya mageuzi ya utendaji kazi na wafanyakazi wakamwelewa hivyo kufanikisha utekelezaji wa mkakati wao wa biashara ulioanza kutekelezwa mwaka mmoja uliopita.
“Alipoingia CRDB hakuja na business as usual. Aliikuta benki ikiwa bora na akataka kuifanya kuwa bora zaidi. Aliileta kauli mbiu ya tupo tayari ambayo wafanyakazi wote tumeielewa na matokeo yanaonekana,” alisema Tully.
Kuhakikisha benki inaendeleza mafanikio yaliyopatikana, alisema mkakati mpya wa biashara umeandaliwa ambao unajikita katika maeneo sita ya kipaumbele.
“Tunasisitiza kuhama kutoka kufanikisha miamala mpaka kushiriki kuujenga uchumi na kuwekeza kwenye vipaji vya watu wetu badala ya kuwatumia. Kwa miaka mitano ijayo, tutajikita kuimarisha ushirikiano na wabia wetu, kuilinda benki na vihatarishi vya aina yoyote pamoja na mazingira. Tunataka kuwa benki kiongozi katika kila kitu tunachokifanya iwe ubunifu na matumizi ya teknolojia, kushiriki miradi ya maendeleo au kuwainua wajasiriamali na kingine chochote,” alisisitiza Tully kuhusu uelekeo wa benki hiyo.
Licha ya benki hiyo kuwa na matawi katika wilaya zote 169 pamoja na takriban mawakala 20,000 wanaofanikisha huduma kwa wastani wa wateja milioni tatu inaowahudumia kila mwezi, Isaac Chacha, mdau wa huduma za fedha alisema itapendeza iwapo kwenye mkakati mpya itatoa nafasi kubwa kwa wajasiriamali wadogo.
“Iangalie namna ya kupunguza masharti kwa wanaoomba mikopo midogo. Iwapo benki itawasaidia wajasiriamali wadogo kukua sio tu ajira zitaongezeka nchini bali wafanyabiashara wakubwa watakuwa wengi hivyo kujihakikishia wateja wengi siku za baadaye,” alisema Chacha.
Ndani ya miaka mitano iliyopita, amana za watwatejaeja wa CRDB zimeongezeka kwa asilimia 88 zikipanda kutoka Sh4.32 trilioni mwaka 2017 mpaka Sh8.14 trilioni mwaka 2022 jambo linalodhihirisha imani yao kwa taasisi hiyo kubwa ya fedha nchini.
“Ukifuatilia unaweza kukuta wateja wengi ni wanawake. Basi CRDB itoe kipaumbele kwetu ikiwezekana ifike mpaka vijijini iangalie namna ya kutuwezesha kwani kuna wakati tunakosa hela ya kununua mbolea na viautilifu. Tukikopeshwa, kilimo chetu kitaimarika,” alisema Meriana Nganyanyuka, mkulima wa korosho mkoani Pwani.