***********************
Na. Damian Kunambi, Njombe.
Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Victoria Mwanziva ameziomba mahakama wilayani humo kutengeza utaratibu wa utoaji elimu ya sheria kwa viongozi wa ngazi ya kata na vijiji ili kuhakikisha wananchi wanapata haki stahiki pindi wapelekapo mashauli yao katika ngazi hizo.
Mwanziva ametoa ushauri huo wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki la sheria nchini na kuongeza kuwa endapo elimu hiyo itatolewa vyema kwa watendaji hao itasaidia kupunguza msongamano wa kesi katika mahakama mbalimbali kwani mashauli mengi yatakuwa tayari yamekwisha malizika katika ngazi hizo za kata na vijiji.
” Napenda kutoa ushauri kwa mahakama wa wilaya ya Ludewa, wapeni elimu ya sheria viongozi wa kata na vijiji ili watoe haki kwa usawa, wakipata elimu hiyo itasaidia kufanya maamuzi sahihi ya kesi za wananchi na kuepusha migogoro ya hapa na pale”, Amesema Mwanziva.
Aidha amewapongeza kwa kuadhimisha wiki hili la sheria kwa kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi wa kata mbalimbali wilayani humo, kushiriki shughuli za kijamii pamoja na michezo ambayo ilihusisha makundi mbalimbali.
Akisoma taarifa ya mwenendo wa mahakama wilayani humo Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Ludewa Isaac Ayeng’o mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Victoria Mwanziva amesema matumizi ya TEHAMA yamesaidia huduma za kimahama kutolewa kwa uwazi, kupunguza gharama kwa wateja wakati wa ufunguaji mashauri, kupata taarifa za mashauri kwa njia ya mtandao pamoja na kufanya malipo ya ada za mashauri kwa kutumia mfumo huo.
“Kupitia mfumo wa TEHAMA mahakama yetu imefanikiwa kusikiliza hukumu mbili kwa njia ya video mtandao (Video Conference) njia ambayo tumeona inasaidia na kuwaepushia usumbufu wananchi”, amesema Ayeng’o.