Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ametoa rai kwa umma kujielekeza zaidi kwenye utatuzi wa migogoro mbalimbali kwa njia ya Usuluhishi ili kukuza uchumi, kuokoa muda na hatimaye kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani.
Akizungumza leo tarehe 01 Februari, 2023 wakati wa hafla ya kilele cha Siku ya Sheria nchini iliyofanyika kitaifa katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma, ambapo Mgeni Rasmi akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Jaji Mkuu amesema kuwa; kwa mwaka huu Mahakama imechagua Kaulimbiu inayohimiza Usuluhishi kama njia mbadala wa kutatua migogoro.
“Usuluhishi unahimizwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama njia bora ya kutatua migogoro kwa haraka na kwa gharama nafuu. Mahakama, Wadaawa na Wadau, wanapotumia njia ya Usuluhishi kutatua migogoro, wanakuwa sio tu wanatekeleza maagizo ya Ibara ya 107A (2) (d) ya Katiba ya Tanzania (1977), bali pia wanatekeleza misingi ya haki nyingine stahiki kwa wahusika wa mgogoro, ambayo ni haki kutocheleweshewa haki bila sababu za msingi inayotambuliwa na Ibara ya 107A (2) (b) ya Katiba,” amesisitiza Mhe. Prof. Juma.
Jaji Mkuu amesema kwamba, ingawa Mahakama ya Tanzania katika Wiki na Siku ya Sheria ilichagua kauli mbiu ya kuhimiza Usuluhishi kama njia mbadala wa kutatua migogoro, lakini pia inaunga mkono kauli iliyotolewa na Rais Samia, mapema mara baada ya kuingia madarakani tarehe 18 Machi 2021, ambapo alihimiza mazungumzo, majadiliano na usuluhishi kwenye migogoro ya kisiasa.
Mhe. Prof. Juma ameongeza kuwa, utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi unafanana na falsafa ya maridhiano, ustahimilivu na mabadiliko ya kujenga upya nchi na kwamba Haki inayopatikana Mahakamani kwa njia ya kawaida inapatikana kwa kupitia ngazi, vituo vingi, mitiririko na misururu ya hatua ambayo huchangia ucheleshwaji na huongeza gharama za kesi.
Akizungumzia Kituo cha Usuluhishi kilichopo chini ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Prof. Juma amesema kuwa Kituo hicho kilianzishwa ili kujenga uzoefu na ufahamu wa kina kuhusu dhana ya Usuluhishi kisha kutumia uzoefu huo kusaidia kurahisisha na kuharakisha utatuzi wa mashauri ya madai yanayofunguliwa, kwa kuanzia, katika Masjala za Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na Divisheni ya Ardhi na vilevile kutumia uzoefu uliopatikana kueneza matumizi ya usuluhishi katika ngazi zote za Mahakama nchini.
Aidha; Jaji Mkuu ameunga mkono hoja iliyotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika hotuba yake aliyowasilisha leo katika hafla hiyo ya kuwa, anafikiria kuwasilisha pendekezo ya Sheria bungeni ya kulazimisha Mashauri yote kupitia hatua ya usuluhishi kabla ya kuanza kwa usikilizwaji wa shauri husika kwa njia ya kawaida.
Jaji Mkuu amebainisha baadhi ya faida za usuluhishi ambazo ni pamoja na; kusaidia kutatua migogoro kwa haraka ambapo inachukua takribani siku 30 kwa shauri la usuluhishi kukamilika, kuleta amani na mshikamano, kukuza uchumi wa nchi na kadhalika.
Aidha; Mhe. Prof. Juma ameiunganisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ambayo pamoja na mambo mengine inalenga pia kuwepo kwa mazingira ya amani, usalama na umoja; utawala bora na utawala wa sheria; uwepo wa jamii iliyoelimika na inayojifunza; na kujenga uchumi imara na shindani.
“Kupitia Dira ya Taifa, Mahakama inaamini kuwa, utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi ni kutekeleza Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya kuwawezesha wananchi wanaohusika na mashauri kutumia muda wao vizuri katika shughuli za kujenga uchumi,” ameeleza.
Kadhalika; Jaji Mkuu amebainisha kuwa, usuluhishi ni muhimu katika kutatua migogoro ya ardhi kwa kuwa migogoro ya aina hiyo ni adui mkubwa kwa maendeleo, amani na ustawi wa wananchi. Ameongeza kuwa, Sheria ya Mahakama za Ardhi, sura ya 216 inatambua umuhimu wa matumizi ya usuluhishi katika utatuzi wa migogoro ya ardhi inayofikishwa mbele ya Mabaraza ya Ardhi ya Vijiji na kwenye Mabaraza ya Kata.
Katika hatua nyingine, Mhe. Prof. Juma amemshukuru Rais Samia kwa uteuzi wa Majaji 22 walioteuliwa tarehe 6 Agosti, 2022 na kuongeza nguvu kazi na hivyo kupunguza mzigo wa mashauri kutoka 340 hadi 265 kwa kipindi hicho. Amekiri kuwa, idadi hiyo imeongeza kasi ya usikilizwaji wa mashauri kutoka asilimia 112 kwa mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 113 kwa mwaka jana.
Mbali na ongezeko la Majaji, Jaji Mkuu amemshukuru Mgeni Rasmi kwa watumishi wapya 292 walioajiriwa wakiwemo Mahakimu Wakazi 48, kukamilisha ujenzi wa Majengo mapya 32, Serikali kuridhia na kufanikisha kuingia katika makubaliano na Benki ya Dunia ya kuongeza fedha na muda wa utekelezaji wa Mradi wa Maboresho.
Kaulimbiu ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria nchini kwa mwaka huu 2023 inasema; “Umuhimu wa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi katika kukuza uchumi endelevu; Wajibu wa Mahakama na Wadau.”
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kituo cha Usuluhishi kilichoanzishwa Julai, 2015 mahsusi kwa ajili ya kusuluhisha mashauri mbalimbali hadi sasa kimepokea jumla mashauri ya usuluhishi 1942, kati ya idadi hiyo jumla ya mashauri 326 yamesuluhishwa na mashauri 20 yamefanikiwa kiasi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (katikati) akisiliza hotuba iliyokuwa ikitolewa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha) wakati wa hafla ya kilele cha Siku ya Sheria nchini. Aliyeketi kulia ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdallah na kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani
Baadhi ya makundi mbalimbali ya Viongozi mbalimbali, Watumishi wa Mahakama pamoja na Wadau wakiwa katika sherehe za kilele cha Siku ya Sheria nchini zilizofanyika leo tarehe 01 Februari, 2023 katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania (kushoto), Viongozi wengine wa Mahakama na wageni waalikwa wakifuatilia yaliyokuwa yanajiri katika hafla ya kilele cha Siku ya Sheria nchini, 2023.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akiwasilisha hotuba yake katika hafla ya kilele cha Siku ya Sheria nchini, iliyoadhimishwa leo tarehe 01 Februari, 2023.
Meza kuu ikiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (katikati) wakiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akikagua gwaride maalum ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa shughuli za Mahakama kwa mwaka huu 2023.