MWAKILISHI wa Viti Maalum Mhe.Amina Idd Mabrouk, akizungumza na Wanafunzi wa Kidato cha Nne wa Skuli ya Sekondari Chukwani waliopo katika kambi ya maandalizi ya kufanya Mitihani ya Taifa ya kidato cha Nne Mwaka huu.
MWAKILISHI wa Viti Maalum Mhe.Amina Idd Mabrouk,(kushoto) akikabidhi Vyakula mbali mbali vikiwemo Mchele, Unga wa Ngano na Mafuta ya kula kwa Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari Chukwani Mohamed Abdallah Mohamed(kulia), kwa ajili ya Wanafunzi waliopo katika kambi ya maandalizi ya Mitihani ya Kidato cha Nne kwa Skuli hiyo.
MWAKILISHI wa Viti Maalum Mhe.Amina Idd Mabrouk,akiwa katika Picha ya pamoja na Wanafunzi wa Kidato cha Nne wanaotarajiwa kufanya Mitihani ya Taifa Mwaka huu.
………………..
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
WANAFUNZI wanaojiandaa kufanya Mitihani ya Taifa ya kidato cha Nne Mwaka huu, Visiwani Zanzibar wametakiwa kusoma kwa bidii ili wafaulu mitihani hiyo.
Wito huo umetolewa na Mwakilishi wa Viti Maalum Mhe.Amina Idd Mabrouk, katika mwendelezo wa ziara zake katika Mkoa wa Magharib, wakati akikabidhi Vyakula mbali mbali kwa Wanafunzi wa Kidato cha Nne wa Shule ya Sekondari Chukwani waliopo katika kambi ya maandalizi ya mitihani kwa mwaka huu.
Mwakilishi huyo amewasihi Wanafunzi hao kusoma kwa bidii ikiwa ni sehemu ya maandalizi rasmi ya kuwawezesha kufaulu.
Alisema wanafunzi hao wakifaulu vizuri watapata nafasi ya kuendelea na masomo ya ngazi za juu hadi kufikia Chuo Kikuu, hatua inayohitaji juhudi binafsi za kila mwanafunzi.
“Elimu ni mkombozi wa maisha ya kila mwanadamu, kumbukeni kuwa nyie ndio wataalamu wa fani mbali mbali wa baadae Taifa linakutegemeeni hivyo ni lazima mtumie muda wenu vizuri kwa ajili ya kutafuta Elimu hadi ngazi za Vyuo Vikuu”, alitoa Nasaha hizo Mwakilishi huyo.
Pamoja na hayo aliwasisitiza wanafunzi hao kuachana na vitendo visivyofaa hasa kushiriki katika masuala ya dawa za kulevya, mahusiano ya kimapenzi katika umri mdogo sambamba na matumizi mabaya ya simu.
Akipokea Vyakula hivyo Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari Chukwani Mohamed Abdallah Mohamed, alishukru kwa msaada huo na kueleza kuwa utawasaidia wanafunzi hao kupata Chakula kwa wakati na kupata muda wa kusoma vizuri katika kambi hiyo.
Mwl.Mohamed, alieleza kuwa Uongozi wa Skuli hiyo umejipanga vizuri kwa kuwaanda vizuri wanafunzi hao 122 wanaotarajiwa kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne kwa Mwaka huu.
Vyakula vilivyotolewa na Mwakilishi huyo ni pamoja na Mchele,Sukari, Unga wa Ngano pamoja na Mafuta ya kula.