Na.Mwandishi Wetu-NJOMBE
Baraza la madiwani la halmashauri ya wilaya ya Njombe limepitisha rasimu ya bajeti ya maendeleo ya bil 30.6 ya halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Wakati bajeti hiyo ikipata baraka za madiwani mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Njombe Valentino Hongoli amesema madiwani wanatakiwa kusimamia vizuri miradi inayoendelea kutekelezwa katika halmashauri hiyo na kutenga fedha asilimia 10 kwa ajili ya mikopo ya vijana, akina mama na watu wenye ulemavu.
Amesema katika kutekeleza miradi ya kimkakati inatakiwa ushirikiano na usimamizi mkubwa wa makusanyo ya mapato na kupeleka fedha kwa wakati katika miradi.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Njombe Sharifa Nabalang’anya amesema kupitia bajeti hiyo halmashauri inatarajia kutekeleza na kubuni miradi mbalimbali ya kimkakati ili kuongeza mapato ya halmashauri.
Amesema kabla ya kupitishwa kwa bajeti hiyo asilimia 70 ya mapato ya ndani yalikuwa yanategemea eneo moja pekee la misitu lakini sasa wanakwenda kuondokana na hali hiyo.
“Kutokana na mafunzo waliyoyapata baada ya kutembelea halmashauri za Chalinze na Dodoma yameleta matokeo makubwa na yameanza kuonekana,alisema Sharifa Nabarang’anya mkurugenzi halmashauri ya wilaya ya Njombe.
Baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo akiwemo Neema Mbanga amesema shule ya secondari Lupembe inakabiliwa na changamoto ya bweni hivyo pamoja na jitihada za wananchi katika kuchangia ujenzi lakini wanahitaji nguvu kutoka serikalini.
“Bweni la sekondari Lupembe nguvu ya wananchi imetumika na maeneo yaliyobakia kama vyoo na rangi wananchi hawawezi ” amesema Mbanga