Na Mwandishi wetu, Simanjiro
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, limewateua Madiwani watatu watakao wawakilisha kwenye Mamlaka ya Mji mdogo wa Mirerani.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Jacob Kimeso, amesema madiwani hao watatu wa kata za Mirerani, Endiamtu na Naisinyai, watawawakilisha kwenye mji huo.
Kimeso amesema mchakato wa kuwapata madiwani hao kwa ajili ya kuwawakilisha kwenye mamlaka ya mji huo, umechukua muda mrefu hivyo suala hilo limefikia tamati hivi sasa.
“Baraza la madiwani limeshawateua na kuwapitisha hivyo, tunawapongeza madiwani hao na tunawatakia kila la heri katika kutuwakisha kwenye mamlaka hiyo,” amesema Kimeso.
Diwani wa kata ya Orkesumet, Sendeu Laizer amesema ni vyema madiwani hao wakatajwa kwa majina kuwa ni Lucas Chimba Zacharia (Endiamtu), Salome Nelson Mnyawi (Mirerani) na Taiko Kurian Laizer (Naisinyai) ili kuhifadhi kumbukumbu sahihi.
“Kuandika madiwani bila kuwatambua kwa kutaja majina yao na kata zao haitakuwa vyema hivyo ili kuweka kumbukumbu sawa inabidi tuwatambue kwa njia hiyo,” amesema Laizer.
Katibu wa UWT Wilaya ya Simanjiro Leokadia Fisoo akizungumza kwa niaba ya uongozi wa CCM wa wilaya ya hiyo ameeleza kuwa ni vyema chama hicho kikapatiwa taarifa rasmi ya suala hilo.
“Viongozi wa CCM wa wilaya ya Simanjiro wamefuatilia suala hili kwa muda sasa hivyo wanapaswa kupewa taarifa ya maandishi ya kuteuliwa kwa madiwani hao,” amesema Fisoo.