Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
MKUU wa mkoa wa Pwani, alhaj Abubakari Kunenge,amewaasa wakuu wa wilaya wasiwe chanzo cha vikwazo, kukwamisha jitihada za Rais dkt Samia Suluhu Hassan,bali wakawatumikie na kuwahudumia wananchi.
Aidha wameaswa kwenda kufanya kazi kwa karibu pamoja na kamati za amani ili kushughulikia na kusimamia kwa pamoja kupunguza masuala ya uhalifu,ubakaji ,ulawiti na mmomonyoko wa maadili ambayo yanaonekana kushamiri.
Kunenge alitoa Rai hiyo Januari 30 baada ya kuwaapisha wakuu wa wilaya wapya wa wilaya ya Mafia na Kibiti .
Vilevile alieleza, Mkoa wa Pwani ni mkoa wa biashara, uwekezaji hivyo wakuu hao wa wilaya wakaweke Mazingira bora ya uwekezaji kuvutia wawekezaji ili pia kuongeza vyanzo vya mapato.
Kunenge pia alifafanua mkoa huo una changamoto ya uvamizi wa Ardhi na changamoto kubwa ya migogoro ya ardhi kwa kutofuata sheria , ambapo amewataka wakatende haki na kusimamia changamoto hizo .
“Tukawatumikie na kutatua kero za wananchi,wakahudumie wananchi sisi ni watumishi wa wananchi, kwasababu CCM iliahidi na wananchi wakaridhia,kuna mkataba wa wananchi na CCM kutekeleza ilani hivyo wajibu wetu ni kutekeleza ilani”anasema Kunenge.
“Pamoja na hayo ,mkafanye kazi na Halmashauri na Taasisi zote za Serikali kusimamia mapato ya halmashauri na kusimamia usiwepo utoroshaji wa fedha za mapato ambao wakati mwingine unafanywa na baadhi ya watumishi”.
“Hakikisheni mnajua wilaya zenu kama viganja vyenu vya mkono,mkajue kero za wananchi wenu na kuwatumikia,tokeni maofisini muende mkajue kero zao na kuzitatua”alibainisha Kunenge.
Mkuu huyo wa mkoa,aliwapongeza wote walioteuliwa na kuhamishiwa Mkoani humo, na amemshukuru Rais kwa uteuzi wake ,Na amewaomba wakuu wa wilaya wote kufanya kazi Kama timu moja kimkoa ili kuinua uchumi wa Maendeleo ya mkoa .
Awali Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani,Zuwena Omari aliwasihi wakuu wa wilaya kijumla kwenda kusimamia mapato na mianya ya utoroshaji wa fedha za mapato ambao wakati mwingine unafanywa na baadhi ya watumishi.
Alizitaka Halmashauri zitumie mashine za kukusanyia mapato kwa njia ya kielektroniki ili kupunguza upigaji wa mapato.
Zuwena alitoa rai pia kusimamia asilimia 10 za Halmashauri ambazo zinatengwa kwa ajili ya vikindi vya vijana, wanawake na makundi maalum.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya Kibiti Kanal Joseph Kolombo na Mafia Zephania Stephan Sumaye walisema wamepokea maagizo waliyopewa na kuahidi kusimamia utekelezaji wa ilani na kuwatumikia wananchi kwa maslahi ya Taifa.