Na Dotto Mwaibale, Mkalama
MWENYEKITI wa Halmashauri ya Mkalama, James Mkwega amewataka watumishi kufanya kazi kwa kushindana kila idara ili kuiletea maendeleo halmashauri hiyo na kuwaondoa hofu kuwa hakuna atakayefukuzwa kazi kama wanajituma kufanya kazi kwa bidii.
Mkwega ameyasema hayo wakati akifungua kikao maalumu cha Baraza la Madiwani la kupitia na kujadili mapendekezo ya bajeti ya kwa Mwaka wa fedha 2023/2024 ambacho kilipitisha bajeti ya zaidi ya Sh. Bilioni 27.
“Watendaji fanyeni kazi kwa ‘kurelax’ hatuna mpango wa kumchukia mtumishi wala kumfukuza ila atakayependa kujifukuzisha mwenyewe tunamruhusu,” alisema Mkwega.
Alisema watumishi wanapofanya kazi na kuleta matokeo chanya ya maendeleo kwa wananchi wanatengeneza historia ambayo hataikitokea amekufa kuna alama ambayo ataiacha ambayo itazungumzwa na walio hai.
“Hapa mnajaziliza historia ili hata mtakapoondoka duniani kunajambo zuri litazungumzwa juu yenu, niwaombe na kuwatia nguvu watumishi jitumeni na endeleeni kufanya kazi kwa kushindana kwa kila idara.
Alisema katika utendaji wa kazi hakuna kitu kinacholeta mgawanyiko kama tafsiri ya ulaji,hivyo nawaomba kwenye ofisi zenu muepukane na jambo hilo.
Aidha, alisema katika mwaka huu wa fedha halmashauri inampango wa kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuwaomba watumishi kushirikiana idara zote ili kufikia malengo ya kukusanya na kutumia zaidi ya Sh.Bilioni 27.
Mkwega alitumia nafasi hiyo kumpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo na timu yake kwa kuandaa bajeti nzuri inayozingatia vipaumbele na mahitaji ambayo ina kwenda kuleta mahitaji ya maendeleo ya wananchi.
Awali akisoma Rasimu ya Mpango wa bajeti, Kaimu Afisa Mipango wa Halmashauri hiyo Daniel Tesha alisema nguvu kubwa wameielekeza katika ukusanyaji wa mapato ambapo wanategemea kuongeza ukusanyaji wa mapato huru ya ndani kutoka Sh. Bilioni 1.287 hadi Sh. Bilioni 1.333 ambazo kati hizo Sh. Milioni 302. 7 zitatumika kwa shughuli za utekelezaji wa miradi ya maendeleo na Sh.Bilioni 1.zitakuwa kwa ajili ya shughuli za uendeshaji.
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Said Kalima alisema atahakikisha bajeti hiyo inakwenda kufanya kazi kwa malengo yaliyokusudiwa.